16 February 2012

Mawaziri: Afrika iko makini na mchakato APRM

Na Mwandishi Wetu

MAWAZIRI kutoka nchi za Uganda na Tanzania, wameungana na wawakilishi 13 kutoka nchi za Afrika kuupongeza Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).

Pongezi hizo zimetolewa Dar es Salaam jana katika mjadala unaohusu APRM jinsi inavyosaidia nchi hizo kunufaika na madini waliyonayo kwenye mkutano wa wataalamu wa nchi za Afrika ambao umeandaliwa na Kamisheni ya Uchumi Afrika (UNECA).

Walisema mpango huo ni chachu kusaidia nchi hizo kuimarisha uchumi na utulivu wa kisiasa.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw.Adam Malima, alisema APRM ni mchakato uliokubaliwa na viongozi wa Afrika kuhusisha wataalamu wao wa ndani na wananchi kusaka majibu ya masuala muhimu.

“Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha nchi yetu inanufaika na madini yake, tumepitisha sera mpya ya madini mwaka 2009 na sheria mwaka 2010 lakini tunahitaji kupata mawazo zaidi juu ya namna tunavyoweza kuendeleza sekta hii, hapa ndipo umuhimu wa APRM unapojitokeza.

“Taasisi hii itatusaidia sana kujitazama kwa kujilinganisha na nchi nyingine za Afrika jinsi zinazofanya kazi,” alisema.

Waziri wa Mipango wa Uganda, Matia Kassaija alisema APRM ni taasisi muhimu katika kulisaidia Bara la Afrika kupata majawabu ya Kiafrika kwa matatizo yao ya ndani.

“Ningependa kupingana na mtoa mada aliyeonesha wasiwasi kama Marais wa Afrika wako makini na mchakato huu, mimi nikiwa Waziri ninayehusika na APRM kule Uganda, naweza kuthibitisha kuwa viongozi wa Afrika wanaheshimu sana mpango huu na wataendelea kuuimarisha,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Bi. Rehema Twalib, alisema APRM ilianzishwa mwaka 2002 na wakuu wa nchi za Afrika kuwa taasisi ambayo itafanya kazi ya kutathmini utawala bora miongoni mwa nchi wanachama ili kuzisaidia nchi moja moja na baadaye bara zima la Afrika.

No comments:

Post a Comment