15 February 2012

UN yazidi kubeba lawama kuhusu Syria

NEW YORK,Marekani

MKUU wa Tume ya Kutetea Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa UN,Bi.Navi Pillay amesema kutokuwepo na msimamo imara kuhusu Syria katika baraza la usalama la umoja huo, kumechangia maafa zaidi ya raia.

Bi. Pillay ameorodhesha aina mbali mbali za ukiukwaji wa haki za binadamu na akasisitiza kuwa amefadhaishwa sana na mashambulizi ya raia katika mji wa homs.

Akizungumza mjini New York jana  alitoa ushaidi kuonesha kuwa majeshi ya Syria yanatekeleza uhalifu dhidi ya binadamu.

"Imekuwa vigumu sasa kwa ofisi yangu kuchukua takwimu ya vifo vilivyo tokea katika kipindi cha miezi miwili. Lakini tuna uhakika kuwa idadi ya waliokufa na waliojeruhiwa inaongezeka kila siku" alisema Bi Pillay

Kamishna huyo, alielezea bayana kuwa amechukizwa na mabalozi wa baraza la usalama la umoja wa mataifa ambao wameshindwa kutoa kauli moja kuhusu Syria.

Alisema kuwa hali hii, imechochea utawala nchini humo kuzidisha mashambulizi dhidi ya upinzani.

Matamshi makali ya Bi Pillay yalilenga kushinikiza utawala wa Rais Assad, Urusi na China ambao walipiga kura ya turufu kupinga mswada huo dhidi ya Syria kwenye baraza la uslama  kubadilisha msimamo,lakini hakuna dalili zozote kuwa matamshi yake yatabadilisha mambo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi,Bw. Sergei Lavrov, ambaye alizuru Syria wiki iliyopita, alisisitiza kuwa suluhu ya mzozo huo itapatikana bila shinikizo kutoka nchi za kigeni.

"Tuna jukumu la kuwasaidia watu wa Syria. Ni kwa sababu hii tunahitaji kupanua majadiliano kati ya raia wa Syria ilikupata suluhu au uamuzi ambao utazingatia matakwa ya raia wote nchini humo bila kuingiliwa na wahusika wengine kutoka nje" alisema Bw Lavrov.

Baraza la usalama linajadili ripoti ya kamishna Bi.Pillay, lakini awali balozi wa Syria katika UN,Bw. Bashar Ja'afari alijaribu kuvunja mkutano huo.

Balozi huyo alipata kuungwa mkono na wenzake kutoka Iran na Korea Kaskazini, lakini mwenyekiti wa baraza hilo alipinga kauli zao.

Bado kuna migawanyiko kwenye baraza hilo kuhusu suala la Syria na awali wanachama walikuwa na tashwishi kuhusu pendekezo la kuudwa kwa kikosi cha kulinda amani kitakacho jumuisha Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za kiarabu nchini Syria.(BBC)


No comments:

Post a Comment