LAGOS,Nigeria
KUNDI la wanamgambo la Boko Haram limesema kuwa limewaua wanajeshi 12 wa serikali baada ya kufanya mashambulizi Kaskazini Mashariki mwa mji wa Maiduguri nchini Nigeria.
Hata hivyo maofisa wa usalama nchini humo wamekana kuuawa kwa wanajeshi hao na badala yake Jeshi la pamoja nchini humo linalojaribu kukabiliana na mashambulizi ya kundi hilo la Boko Haram Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo lilisema wao ndio waliofanikiwa kuuwa wanachama 12 wa Boko Haram na kuwa wanajeshi wake wawili walijeruhiwa tu na sio kuuawa.
Kundi hilo la Boko Haram lilianza mashambulizi yake kwa mara ya kwanza mwaka wa 2003 nchini Nigeria.
Msemaji wa kundi hilo,Bw. Abul Qaqa aliwaambia wanahabari kwamba wamefanya mashambulizi hayo baada ya kuuwa watu watatu wanaodai wanatoa habari za kundi hilo kwa polisi.
Katika hatua nyingine, Shirika la kimataifa la mabaharia limesema maharamia nchini Nigeria wameshambulia meli moja ya mizigo na kumuuwa nohodha wa meli hiyo pamoja na mhandisi wake mkuu.
Kulingana na taarifa za shirika hilo, maharamia waliokuwa na bunduki waliifuatilia meli hiyo ya MV Forces na kuwafyatulia risasi abiria na kusababisha vifo vya watu hao wawili huku wengine wakijeruhiwa.
Shirika hilo la IMB linaamini kuwa maharamia hao ni raia wa Nigeria.
Vikosi vya kulinda doria baharini na jeshi la Ufaransa lilisaidiana kuokoa manusura wengine waliokuwa wamejifungia katika maeneo salama ndani ya meli iliyoshambuliwa.
Hata hivyo msemaji wa jeshi la wanamaji nchini Nigeria Bw. Kabir Aliyu alithibitisha shambulizi hilo.
Shambulizi hilo limetokea wakati ambapo viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi wakitarajiwa kukutana kuzungumzia suala la maharamia, mkutano utakaofanyika katika mji mkuu wa Nigeria Abuja.(BBC).
No comments:
Post a Comment