13 January 2012

Athali za Mfumuko wa Bei

Na Makumba Mwemezi

Mwaka 2012 huwenda ukawa mgumu zaidi kwa watanzania hasa wenye kipato cha chini, kutokana na Serikali kushindwa kudhibiti mfumuko wa bei ambao umepelekea benki za biashara kupandisha viwango vya riba za mikopo kutoka wastani wa asilimia 23 Mwishoni mwa mwaka jana hadi wastani wa asilimia 45 kuanzia Januari Mwaka huu.
Taarifa kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa zinaonesha kuwa Mfumuko wa Bei umezidi kuongezeka kutoka chini ya asilimia 5 mwanzoni mwa mwaka jana hadi asilimia 19.2 mwishoni mwa Mwezi Novemba 2011, na kuathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa shilingi katika kufanya manunuzi.

Kupanda kwa viwango vya riba za mikopo katika mabenki ya biashara si tu kuwa kutaathiri mwenendo wa urejeshaji mikopo iliyokwisha chukuliwa bali kutapunguza pia kasi ya ukopaji mpya hivyo kuathiri biashara za kibenki na uwekezaji.

Akizungumza na Majira katika mahojiano maalumu, Mwenyekiti wa Chama cha wenye Mabenki Tanzania na ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Tanzania, Lawrence Mafuru amethibitisha kupanda huko kwa viwango vya riba za mikopo ya benki na kuutaja mfumuko wa bei kuwa chanzo kikubwa.

Kwa Mujibu wa Mafuru sababu nyingine ambazo zimechangia ongezeko hilo ni pamoja na hatua ya serikali ya kuondoa kiasi cha zaidi ya bilioni 100 katika mzunguko wa fedha kama njia ya kudhibiti mfumuko huo, hatua ambayo imezipunguzia benki uwezo wa kukopesha kwa kukosa fedha za kutosha.

Serikali pia imeongeza viwango vyake vya amana (Deposit) zisizotozwa riba kutoka asilimia 20 mpaka 30 jambo ambalo pia linafanya kiasi kikubwa cha pesa kutokuwa katika mzunguko wa kawaida hivyo kuzikosha benki uwezo wa kukopesha na kuzalisha faida.

Aidha Mafuru alisema viwango vya kukopeshana miongoni mwa mabenki pia vimepanda kutoka wastani wa asilimia 5 mwanzoni mwa mwaka jana mpaka wastani wa asilimia 30 Mwaka huu jambo ambalo linalazimisha pia viwango vya riba za mikopo kwa wateja wao ziongezeke.

"Unaweza kuangali jinsi ambavyo mfumuko wa bei na hatua zinazochukuliwa na serikali kuudhibiti vilivyochangia kuongeza ghalama za uendeshaji wa benki, lakini pia benki zinapata pesa kwa riba ya juu kutoka vyanzo vyake, unadhani hataungelikuwa wewe unaendesha biashara hii ungechukua hatua gani" anasema Mafuru.


Hatahivyo baadhi ya wataalamu na wachambuzi wa mambo ya uchumi wamesema kama serikali na benki wakiacha viwango hivi viendelee bila kuchukua hatua ya kuvidhibiti, kutakuwa na athari hasi katika uchumi wa taifa ikiwamo kushuka kwa ukopaji na urejeshaji wa mikopo.

Bw. Adrian Njau ambaye ni mchumi katika Baraza la Biashara la Afrika Mashariki, anasema athari za muda mrefu za kushuka kwa urejeshaji mikopo na ukopaji ni benki kutopata faida, kupungua kwa uwekezaji na ufanyaji biashara, kupungua kwa ajira pamoja na kuzorotesha hali ya ukuaji wa uchumi.

"Unaweza kufikilia matokeo ya watu kushindwa kufanya biashara na kuwekeza, watu kukosa ajira na kuporomoka kwa uchumi, hapo ndipo unaweza kugundua kuwa Mwaka 2012 unaweza kuwa wa taabu kwa watanzania wengi kama serikali isipochukua juhudi za makusudi kudhibiti hali hii inayoendelea" anasema Bw. Njau.

Bw. Njau anasema jukumu kubwa ililonalo serikali katika mwaka huu ni kudhibiti mfumuko wa bei, kwa vile kama utaendelea kupanda vipato vya watabnzania waliowengi vitazidi kupungua na watu watazidi kuondoa fedha zao katika mabenki na mzunguko hivyo kuua kabisa uchumi.

Lakini baadhi ya wananchi na wachambuzi wa mambo ya uchumi wanaamini kuwa hatua ya mabenki kupandisha riba za mikopo haitokani na mfumuko wa bei, bali ni ujanja wa kujiongezea faida na kukwepa wajibu wao wa ufuatiliaji urejeshaji wa mikopo.

Msahuri wa maswala ya biashara Bw. Theodory Kaijanante anasema benki zimesahau wajibu wao wa kuhakikisha wanakopesha na kufuatilia uwekezaji wa mikopo hiyo pamoja na urejeshaji jambo ambalo limesababisha wakopaji wengi kukimbia au kushindwa kurejesha mikopo hiyo.

Alisema baada ya kuona hali hiyo benki zimeamua kuongeza viwango vya riba ili kufidia baadhi ya fedha ambazo hazikurejeswa na baadhi ya wakopaji.


"Pamoja na mambo yote wanayotaja kuwa ndio sababu ya upandishwaji wa viwango vya riba, bado benki zinawza kuwa na mchango katika kupunguza viwango hivyo kama zitajikita katika kuwasimamia wakopaji ili waweze kuzalisha na kurejesha mikopo yao kwa wakati na kwa mujibu wa makubalianoa" anadai Kaijanante.

Wadau hawa wanatoa wito kwa serikali kufikili njia sahihi za kudhibiti mfumuko wa bei na kupanda kwa ghalama za maisha badala ya kuondoa fedha katika mzunguko njia mabayo Bw. Mafuru haridhishwi nayo.

Bw. Mafuru anasema tafsiri sahihi ya mfumuko wa bei ni kuwa fedha ni nyingi katika soko kuliko bidhaa za kununua, na njia pekee ya kudhibiti hali hii sio kuondoa fedha katika mzunguko bali kuongeza uzalishaji ili pesa ipate matumizi.

"Serikali inapaswa kufikilia jinsi ya kukuza uzalishaji na kuimarisha uchumi, hivi ndivyo vitaimarisha mfumuko wa bei badala ya kujikita katika mfumuko wa bei ambao matokeo yake ni kuporomosha uchumi kwa ujumla" anasema Bw. Mafuru.

No comments:

Post a Comment