Na Amina Athumani
SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), limesema Chama cha Mpira wa kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD) hakikujiandaa vyema kushiriki michuano ya Taifa inayoendelea
Dar es Salaam ndiyo maana ikazitoa timu zake, si kweli kwamba wamenyimwa posho.
BD imeziondoa kwenye michuano hiyo timu zake za Dar es Salaam ambazo zilikuwa zikiwakilishwa na Wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni kwa madai kuwa TBF haijazipa posho kama ilivyofanya kwa timu mikoani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Msaidizi wa TBF Michael Maluwe, alisema hakuna hata mkoa mmoja uliopatiwa posho za wachezaji kama BD na timu zao wanavyodai.
Alisema kutokana na udhamini uliotolewa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wa sh. milioni 28 kwa ajili ya michuano hiyo, waliamua kuzipunguzia makali timu za mikoani kwa kuzisaidia malazi kwa timu iliyopungukiwa na si posho kwa wachezaji.
"BD na timu zao hawakuwepo kwenye urodha ya kupunguziwa makali kwa kuwa wao ni wa hapa hapa, lakini tuliamua kuwapa sh. milioni 2 ili nao wazibe mapengo kutokana na ufadhili wenyewe tuliopata, lakini cha ajabu walizikataa na tulipowauliza walikuwa na kiasi gani ili tuwaongeze hawakuwa na fedha yoyote," alisema Maluwe.
Alisema kujitoa kwao hakuna tofauti na timu zilizoshindwa kufika kushiriki mashindano hayo, kutokana na maandalizi kama ilivyo kwa Arusha na mikoa mingine na hakutakuwa na adhabu yoyote itakayotolewa dhidi yao.
Michuano hiyo ya kikapu, ambayo imeingia siku ya tatu inafanyika katika viwanja viwili vya Donbosco na Leaders.
Katika mechi zilizochezwa juzi jioni na jana asubuhi, timu za Zanzibar zimeendelea kutakata ambapo Pemba, iliichakaza Shinyanga kwa pointi 118-82 katika mechi ya wanaume na Pemba wanawake, wakailaza Tanga kwa pointi 68-58.
Katika mchezo mwingine, kilimanjaro ambayo imeleta chipukizi kutoka Shule za Sekondari, imeendelea kuchapwa baada ya Tanga kuinyuka kwa pointi 114-07, Shinyanga nayo imeionesha kazi Rukwa kwa kuichapa pointi 62-19, Mara ikaichapa Lindi kwa pointi 50-29 huku, Mbeya ikiiadabisha Mrorogoro kwa pointi 62-41.
Michuano hiyo itaendelea tena leo na itafikia kilele chake Jumamosi.
No comments:
Post a Comment