15 December 2011

Risasi 691 za SMG zaokotwa kaburini

Na Patrick Mabula, Kahama

RISASI 691 za bunduki aina ya SMG, zimekutwa katika moja ya makaburi yaliyopo Mtaa wa Nyihongo, mjini Kahama, mkoani Shinyanga zikiwa zimefichwa katika mfuko wa plastiki.
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana saa saba mchana baada ya wananchi waliokuwa wakichimba kaburi, kuona mfuko huo jirani na eneo walilochagua kumzika ndugu yao.

Wakielezea namna walivyoziona risasi hizo, wananchi hao walisema wakati wakiendelea na kazi ya kuchimba kaburi, waliuona mfuko huo ukiwa umewekwa kwenye kaburi ambalo lilikuwa wazi.

“Katika kaburi hili, kulikuwa na maiti ya mtoto ambayo ilifungwa sanda na kuachwa bila kufukiwa, tulipojaribu kusogelea, tuliona pembeni ya maiti kuna mfuko wa rambo hivyo tuliamua kutoa taarifa polisi,” alisema Bw.Maganga Kapela na kuongeza kuwa, baada ya askari kufika eneo hilo, walikuta risasi katika mfuko huo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Diwani Athuman, amethibitisha kuokotwa risasi hizo na kuwasihi wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo pamoja na kuwa waangalifu katika maeneo ya makaburi na vichaka.

Pia aliwaomba wananchi wasisite kutoa taarifa za siri juu ya watu wanaowatilia shaka ambao pengine wanahusika na vitendo vya uhalifu ukiwemo ujambazi wa kutumia silaha ili kulinda amani.

No comments:

Post a Comment