Na Esther Macha, Mbeya
MBUNGE wa Jimbo la Mbarali, mkoani Mbeya, Bw.Dicksoni Kirufi, amekanusha kuhusika na tukio la uchomaji moto gari la Ofisa Mtendaji Kata ya Ruiwa, wilayani humo, Bw.Jordan Masweve,
kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Bw.Kirufi alikanusha madai hayo jana kutokana na taarifa zinazoenezwa na baadhi ya watu kuwa amehusika na tukio hilo kwa sababu Bw.Masweve, aliwahi kumshtaki mahakamani kwa madai ya kutishia kumuua.
Akizungumza na Majira kwa njia ya simu akiwa mjini Dodoma, Bw. Kirufi alisema tangu amalize kikao cha Bunge hivi karibuni, hajarudi jimboni kwake kwa sababu ya kubanwa na masomo katika Chuo cha Homboro akisomea mambo ya utawala.
“Hapa nilipo sifahamu lolote, nasikia tu kuwa nimeshiriki katika tukio la uchomaji moto gari la Bw.Masweve, kimsingi toka Bunge liishe, sijakanyaga Mbeya nipo masomoni.
“Ujumbe ambao unadaiwa ulikutwa eneo la tukio ukinihusisha mimi si kweli kabisa, nimeshangazwa na taarifa hizi kwa sababu muda wote nipo chuoni nafanya mitihani,” alisema Bw.Kirufi.
Aliongeza kuwa, yeye ni kiongozi makini ndiyo maana wananchi walijenga imani naye na kumchagua kuwa mbunge wao hivyo hawezi kujenga chuki au uhasama na mtu yeyote kwa sababu kama ni masuala ya mahakamani yaliisha na hawezi kulipiza kisasi.
Usiku wa kuamkia Desemba 11, mwaka huu, watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwa Bw. Masweve na kuchoma gari lake lenye namba za usajiri T 574 BFD aina ya Canter.
Katika maelezo yake, Bw. Masweve alisema wakati watu hao wakichoma gari hilo, alishtuka na kukuta matairi yakiteketea kwa moto pamoja na bodi ya gari.
Alisema baadhi ya watu walioshiriki katika tukio hilo aliwaona kwa macho lakini kwa kuwa suala hilo limefika ngazi ya kisheria, polisi watachukua hatua zinazostahili.
Mapema mwezi Oktoba mwaka huu, Bw.Masweve, alimshtaki Bw. Kirufi mahakamani kwa madai ya kutishia kumuua.
Kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya ambapo Bw.Kirufi alipatikana na hatia hivyo mahakama ilimuhukumu kifungo cha miezi 10 jela au kulipa faini ya sh.500,000 ambazo alilipa na kuachiwa huru.
No comments:
Post a Comment