*Amtaka apunguze uzito
Na Zahoro Mlanzi, aliyekuwa Mlandizi
KOCHA Mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, Kostadin Papic ameridhishwa na kiwango cha kiungo wake, Athuman Idd 'Chuji', kwa
kusema sasa amerudi katika kiwango anachokitaka.
Kiungo huyo ambaye amesajiliwa katika dirisha dogo la usajili akitokea kwa watani wao wa jadi, Simba inadaiwa hakuweza kulishawishi benchi la ufundi la timu hiyo, hivyo kuamua kumuacha.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa kirafiki kati ya timu hiyo na Ruvu Shooting, uliopigwa juzi Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, Papic alisema Chuji ni kiungo mzuri na jinsi anavyocheza ndivyo ninavyotaka.
“Chuji amerudi katika kiwango chake cha kawaida, na nina imani kadri tutakavyokuwa tunampa nafasi ya kucheza hususani kipindi hiki cha maandalizi katika mechi za kirafiki, atakuwa mzuri zaidi,” alisema Papic baada ya kuuliza kiwango cha Chuji alivyokiona katika mchezo huo.
Alisema licha ya kwamba amecheza dakika 45 za kipindi cha pili lakini ameonesha kwamba ana vitu tofauti na kubwa zaidi itabidi ampate mazoezi ya kupunguza mwili ili awe mzuri zaidi.
Akizungumzia mchezo huo, Papic alisema timu yake imecheza vizuri kwa kushirikiana na kila mchezaji ameonesha uwezo mzuri kutokana na aina ya wachezaji alionao mabpo kila mmoja anataka kuonesha ana uwezo zaidi ya mwenzake.
Katika mchezo huo, bao la Yanga lilifungwa na Keneth Asamoah na lile la kusawazisha la Ruvu Shooting lilifungwa na Seif Khatibu ambapo Yanga ilichezesha timu mbili.
Timu ya kwanza iliundwa na Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Bakari Mbegu, Nadir Haroub 'Canavaro', Godfrey Bonny, Nurdin Bakari, Juma Seif, Asamoah, Pius Kisambale na Kigi Makasi/
Baada ya mapumziko, kikosi hicho kilitoka na kuingia Hamad Wazir, Salum Telela, Oscar Joshua, Chacha Marwa, Chuji, Shamte Ally, Omega Seme, Jerryson Tegete, Atupele Green na Idrisa Rashid.
No comments:
Post a Comment