29 December 2011

Mgomo wa mafuta sasa wahamia Kilimanjaro

Na Heckton Chuwa, Moshi

SIKU chache baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja kuitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), iwaadhibu kwa kifungo na
kuwanyang’anya leseni wafanyabiashara ambao watafanya hujuma katika usambazaji na uuzaji mafuta nchini, bidhaa hiyo jana iliadimika Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro na kusababisha adha kubwa ya usafiri kwa wannchi.

Majira lilishuhudia magari mengi yakiwa yamepanga foleni katika Kituo cha Gapco, kilichopo Barabara ya Sokoine, eneo la Stendi Kuu, ambacho ndio pekee kilikuwa kikiuza mafuta mjini hapa.

Wakizungumzia adha hiyo, baadhi ya madereva wa magari na wananchi, waliiomba Serikali iwachukulie hatua wafanyabiashara waliofanya mgomo baridi wa kuuza bidhaa hiyo na kukaidi agizo la Bw. Ngeleja.

“Kipindi hiki Mkoa huu huwa na idadi kubwa ya watu ambao wanakuja kula sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya hivyo ukosefu wa mafuta katika vituo, umesababisha adha ya usafiri kwa wananchi.

“Kwanini wafanyabiashara waichezee Serikali, umefika wakati wa kuchukua hatua kwa vitendo ili iwe fundisho kwani bila kufanya hivyo, hali hii itaendelea siku zijazo,” alisema mkazi wa mji huo aliyejitambulisha kwa jina la Bw. John Mushi.


Baadhi ya watu katika eneo la Mbuyuni, Kata ya Bondeni, walikuwa wakiuza mafuta ya petroli na dizeli sh. 2,500 hadi 3,000 kwa lita moja ambapo bei hizo zililalamikiwa na wamiliki wa vyombo vya usafiri.

Uchunguzi uliofanywa na Majira ulibaini kuwa, waendesha pikipiki za abiria 'Bodaboda', walisitisha biashara ya kubeba abiria na kuuza mafuta hayo kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri lakini haikufahamika mara moja mafuta hayo walikuwa wakiyatoa wapi.

Kuanzia saa saba mchana, baadhi ya vituo vilianza kuuza bidhaa hiyo ambapo wamiliki wa vituo vingine walisema kuwa, si kweli kwamba wanafanya mgomo baridi wa kutouza mafuta bali bidhaa hiyo imewaishia katika vituo vyao.

Juhudi za kumpata Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Leonidas Gama, ili azungumzie hali hiyo hazikufanikiwa kwa sababu alikuwa nje ya Mkoa.

Hivi karibuni, wafanyabiashara wa mafuta jijini Dar es Salaam, walifanya mgomo baridi uliodumu kwa siku tatu mfululizo na kusababisha adha kubwa ya usafiri kwa wakazi wa jiji hilo.

Kutokana na hali hiyo, Bw. Ngeleja alisema Serikali imevumilia kwa muda mrefu tabia mbaya za baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta kuhujumu sekta hiyo kila inaposhuka bei.

Alisema leseni walizopewa wafanyabiashara hao ni halali zenye masharti na taratibu ambazo ziko wazi na moja ya sharti hilo ni kuhakikisha mfanyabiashara haleti usumbufu katika sekta hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Bw. Haruna Masebu, alisema mamlaka hiyo imepokea maelekezo ya Bw. Ngeleja na yatafanyiwa kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu.

No comments:

Post a Comment