14 December 2011

Chalenji Cup yaingiza mil. 267/-

 Na Zahoro Mlanzi
* Yaitia hasara SBL

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetangaza mapato ya jumla yaliyopatikana katika michuano ya Chalenji Cup, iliyomalizika wiki iliyopita Dar es Salaam ambapo yameingiza sh. milioni 267,066,000.

Kutokana na mapato hayo, wadhamini wa michuano hiyo Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), kupitia bia yake ya Tusker imepata hasara kubwa kutokana na kutumia sh. milioni 850 katika michuano hiyo iliyokuwa na bajeti ya sh. bilioni 1.2 licha ya kwamba michuano hiyo imefanikiwa.

Mbali na hasara hizo, mchezo ambao uliweza kuvuta mashabiki wengi ni ule uliowakutanisha wenyeji Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) dhidi ya Rwanda 'Amavubi', ambao umeingiza sh. milioni 64,178,000 na ambao uliingiza fedha kidogo ni kati ya Uganda 'The cranes' na Somalia ambazo ni sh. 446,000.

Akitangaza mapato hayo Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ilishirikisha timu za mataifa 12 ambapo hatua ya makundi iliingiza sh. 145,613,000.

“Robo na nusu fainali ziliingiza sh. milioni 58,470,000 na sh. milioni 55,787,000 tofauti wakati fainali iliingiza sh. milioni  17,196,000 na mashabiki walioshuhudia mechi zote walikuwa 103,312, mashabiki 65,617 kati yao walishuhudia hatua ya makundi, mashabiki 17,844 robo fainali, mashabiki 16,014 nusu fainali na mashabiki 4,837 fainali,” alisema Wambura.

Alisema mechi iliyokuwa na washabiki wengi zaidi ni kati ya Kilimanjaro Stars na Rwanda ambapo waliingia 23,946 wakati iliyoingiza wachache ni 446 walioshuhudia mechi kati ya Somalia na Uganda.

Mbali na hilo, Wambura aliwashukuru wadhamini wakuu, Tusker na washabiki waliojitokeza kushuhudia michuano hiyo, Kampuni ya mafuta ya Gapco, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na PSPF na pia wadau wengine waliofanikisha mashindano hayo kwa njia mbalimbali, akiwemo Zacharia Hanspope.

Katika michuano hiyo, Uganda ilitwaa ubingwa kwa mara ya 12 ikifuatiwa na Rwanda na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Sudan, huku wenyeji wakitoka kapa kwa kushika nafasi ya nne.

No comments:

Post a Comment