Na Amina Athumani
CHAMA cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD,) leo kinatarajia kukutana na klabu zote zinazoshiriki Ligi ya Kikapu ya RBA katika Ukumbi wa
Donbosco, Dar es Salaam kupanga mambo mbalimbali ya ligi hiyo.
RBA imepangwa kuanza Januari 7, mwakani baada ya kuahirishwa Desemba 24, mwaka huu ili kupisha sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa BD, Richard Jules alisema mambo yatakayoyazungumzwa ni ada ya ushiriki kwa klabu, kabla ya tarehe ya mashindano hayo kuanza.
"Pia tutazungumzia suala zima la wadhamini katika ligi hiyo, ambapo pia mchakato mzima wa ratiba ya mashindano haya kwa kuwa michuano hiyo, huchezwa kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na wingi wa timu zilizopo katika Mkoa wa Dar es Salaam," alisema Jules.
Alisema maandalizi yamekamilika na timu zitakazoshiriki ni Savio, Vijana, ABC, Oilars, JKT, Pazi, Chui, Hooplife, UDSM Opsider, Polisi, Magone, Prisons, Chang'ombe United na PT.
Jules alisema ndani ya timu hizo baadhi ya klabu zina timu za wanawake na wanaume, hivyo kunaifanya ligi hiyo kuwa ndefu kuliko ligi za mikoa mingine.
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo ni Savio, ambayo wanalishikilia taji hilo kwa muda mrefu sasa.
No comments:
Post a Comment