11 October 2011

TFF yasubiri ripoti ya Poulsen

Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linasubiri ripoti ya Kocha Mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Jan Poulsen, itakayoelezea majumuisho ya matokeo ya
mechi zote zilizokuwa za kuwania kufuzu kucheza mashindano ya Mataifa ya Afrika, mwakani (CAN 2012) ili kujua wapi waboreshe.

Timu hiyo juzi usiku, ilizimwa ndoto zake kushiriki kwa mara nyingine michuano hiyo tangu ipite miaka 20, baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-1, kutoka kwa wenyeji Morocco.

Akizungumza na Waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Angetile Osiah, alisema wameyapokea matokeo hayo kama changamoto, ambapo wanatakiwa kujua wapi walipojikwaa ili mashindano yajayo wafanye vizuri.

"Ukiwa mwanamichezo, upo tayari kupokea matokeo yoyote, hivyo TFF tunayapokea kama yalivyo, lakini tunasubiri kocha awasilishe ripoti yake ambayo itakuwa na kila kitu, kwani itaelezea kwanini hatukufuzu na nini cha kufanya," alisema Osiah na kuongeza;

"Ripoti hiyo atawasilisha katika Kamati ya Ufundi ya shirikisho hilo ambayo itaipitia na kutoa mapendekezo yake kwa kuiwasilisha kwa Kamati ya Utendaji ambayo yenyewe itatekeleza yaliyopendekezwa na kamati hiyo," alisema.

Aliulizwa swali kuhusu uwezo mdogo wa kocha na kwanini wasimfukuze kwakuwa hakufanikiwa kuipeleka timu katika fainali hizo zitakazofanyika katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon, Osiah alijibu; kocha hufukuzwa kutokana na sababu za msingi na pia mkataba unavyoelekeza jinsi anavyotakiwa kufanya kazi yake.

Alisema licha ya kwamba, nchi haikufuzu ni lazima atawasilisha ripoti yake, ambapo sababu inaweza ikawa maandalizi hayakuwa yakutosha, hivyo wanasubiri ripoti na mambo mengine yatafuata.

Alisema baada ya kuondolewa katika mashindano hayo, nguvu zao wanazielekeza katika kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia, ambapo Novemba 11, wataanza kwa kucheza na Chad ugenini.

1 comment:

  1. Watu badala ya kuongolea matayarisho mabovu ya timu hii ikiwa pamoja na kupata michezo ya kutosha kwa ajili ya kujipima nguvu wanaanza kusema eti kocha afukuzwe.Hata akija Pele leo hii kama matayarisho ni mabovu hatutaweza kufanya kitu cha maana hata siku moja.Yaani kwa maandalizi yetu ya kila siku ni sawa na bondia anayejitayarisha kwenda kupigana na Tyson alafu anajipima nguvu kwa kupigana na Maneno Oswald.Tutaishia kuongea kila siku na hakuna cha maana kinachofanyika.Kazi kubwa ya tff ninayoiona kila siku ni wao hodari sana kupanga viingilio katika michezo mikubwa na hakuna lingine la maana wanalofanya.

    ReplyDelete