Na Zahoro Mlanzi
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imeitaka Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa Mara (FAM), kuhakikisha
inakidhi matakwa na taratibu za uchaguzi na si vinginevyo.
Kutokana na hilo, kamati hiyo imeagizwa kuhakikisha waombaji walipe ada za maombi kwa mujibu wa ibara ya 10 (2)(a) na (b), fomu zote za maombi ziwasilishwe kwa katibu wa kamati na iwe inatoa fursa ya pingamizi kwa waombaji.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Angetile Osiah, alisema katika kikao cha pamoja kilichofanyika Oktoba 5, mwaka huu mjini Musoma, kati ya wajumbe wa FAM na wa kamati ya TFF, ilibainika kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi huo.
"Kuna mambo mengi ambayo yamebainika katika kikao hicho, ambapo kamati ya FAM imekiuka baadhi yake, tumeiagiza kamati hiyo kuweka wazi kwenye mbao za matangazo majina ya waombaji wote," alisema Osiah.
Alisema kamati hiyo ya FAM inatakiwa katika kipindi kisichozidi siku tatu kabla ya siku ya mwisho ya uchaguzi, ifanye usaili kwa waombaji uongozi na kutoa uamuzi na kutangaza matokeo hayo.
Pia, kamati hiyo itoe fursa kwa waombaji kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa kamati ya FAM kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, ambapo iweke pia muda maalum wa kupokea rufani hizo.
Aliongeza kwamba, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF katika ibara ya 10(6) na 26(2), uchaguzi wa viongozi wa chama hicho utafanyika Novemba 13, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment