11 October 2011

Poulsen ageukia Kombe la Dunia

*Ni baada kupigwa kumbo CAN 2012

Na Zahoro Mlanzi

SAA chache baada ya kushuhudia timu yake ikishindwa kukata tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwakani (CAN 2012), Kocha Mkuu wa timu ya
Taifa (Taifa Stars), Jan Poulsen amewataka wachezaji wa timu hiyo kutokata tamaa, kwakuwa walicheza na timu bora kuliko wao na zaidi, waangalie mashindano yaliyo mbele yao.

Kauli hiyo imekuja baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 3-1 na Morocco, katika mchezo uliopigwa juzi mjini Marrakech nchini humo, na kuifanya Taifa Stars imalize Kundi D ikishika mkia kwa pointi zake tano.

Kwa matokeo hayo, Morocco 'Simba wa milima ya Atlas', imefuzu kwa kujikusanyia pointi 11, ikifuatiwa na Algeria na Jamhuri ya Afrika ya Kati zikiwiana kwa pointi nane, lakini zikitofautina kwa mabao.

Algeria ilifikisha pointi hizo baada ya juzi kuifunga Afrika ya Kati mabao 2-0, ushindi ambao haukuweza kuisaidia timu hiyo kufuzu, labda Stars kama ingeifunga Morocco na zote kuwa na pointi nane, hivyo utofauti wa mabao ungeangaliwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, ambaye alikwenda na timu nchini humo, ilieleza kwamba, mara baada ya mchezo huo, Poulsen alisema hivi sasa wanatakiwa kuelekeza akili kwenye mechi mbili zilizo mbele yao dhidi ya Chad.

"Mechi hizo za mchujo kwa ajili ya kuingia hatua ya makundi ya mchujo Kanda ya Afrika, ni za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil mwaka 2014, zitachezwa Novemba 11, mwaka huu jijini Ndjamena na marudiano ni Novemba 15, mwaka huu jijini Dar es Salaam," ilieleza sehemu ya taarifa ya Wambura.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mchezo huo wa juzi ambao ulipigwa Uwanja wa Grand, ulimalizika kwa Taifa Stars kufungwa mabao 3-1, ambapo wenyeji waliongozwa na maelfu ya watazamaji, waliokaa vitini ni 43,000, hadi mapumziko timu hizo zilifungana bao 1-1.

Wenyeji Morocco ndiyo walioanza kupata bao dakika ya 19, lililofungwa na Marouane Chamakh kwa mpira wa kichwa, ambao ulidunda kabla ya kumpita kipa Juma Kaseja na kujaa wavuni.

Stars ilisawazisha bao hilo dakika ya 40 kupitia kwa Abdi Kassim 'Babi', kwa shuti kali la umbali wa meta 35, lililomshinda kudaka kipa Nadir Lamyaghri na mpira kujaa wavuni, kufuatia pasi ya Idrisa Rajabu.

Mabao mengine ya Morocco yalifungwa dakika ya 68 na Adel Taarabt na Mbark alifuta matumaini ya Stars kupata sare katika mechi hiyo kwa bao lake la tatu dakika ya 90 kwa shuti la chini akiwa ndani ya eneo la hatari.

Katika mchezo huo, mwamuzi Bakary Gassema kutoka Gambia, aliwaonya kwa kadi za njano Idrisa Rajab, Juma Nyoso, Dan Mrwanda na Mohamed Rajab wa Stars.

Kwa upande wa Morocco aliyeoneshwa kadi ya njano, alikuwa nahodha wa timu hiyo, Houcine Kharja.

Taifa Stars inatarajiwa kurejea Dar es Salaam leo saa 2.30 ndege ya Qatar Airways.

Taifa Stars; Juma Kaseja, Erasto Nyoni/Nassoro Cholo, Idrisa Rajab, Juma Nyoso, Aggrey Morris, Shabani Nditi, Dan Mrwanda, Henry Joseph, Mbwana Samata/John Bocco, Abdi Kassim na Mohamed Rajab/Mrisho Ngasa.

Morocco; Nadir Lamyaghri, Michael Basser, Abdelhamid El Kaoutari, Badri El Kaddouri, Mehdi Benatia, Younes Belhanda, Houcine Kharja, Mbark Boussoufa, Adel Taarabt/Youssef El Arabi, Marouane Chamakh/Said Fettah na Oussama Assaidi/Karim Al Ahmadi.

No comments:

Post a Comment