12 October 2011

TBL yazindua mashindano ya mitumbwi

Na Zahoro Mlanzi

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Balimi Extra Lager, imezindua rasmi mashindano ya mitumbwi kwa mwaka huu, ambapo bingwa kwa wanaume
atapata sh. milioni 2.6 na kwa wanawake sh. milioni 2.2.

Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, Meneja wa bia hiyo, Edith Bebwa, alisema mashindano hayo ya kupiga kasia yatashirikisha mikoa ya Kigoma, Mwanza, Mara, Kagera na visiwa vya Ukerewe, ambapo katika miaka ya hivi karibuni yamekuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa.

Alisema tangu yaanzishwe mashindano hayo, ni zaidi ya miaka sita, huku bia hiyo ikiendelea kudhamini katika mikoa hiyo, ambapo wamefanikiwa kutoa changamoto katika upigaji wa makasia na kujipatia fedha kutokana na zawadi wanazopata washindi.

"Kama ilivyo kawaida, mashindano haya yatatanguliwa na burudani mbalimbali za uhamasishaji, zikifuatiwa na mashindano katika hatua ya mwanzo, kabla ya fainali kuu itakayofanyikia jijini Mwanza Desemba 18, mwaka huu," alisema Edith.

Alisema katika hatua za awali, mashindano yataanzia Kituo cha Mwanza Oktoba 23, mwaka huu, Kigoma na Kagera Novemba 5, Mara na Ukerewe itakuwa Novemba, 19.

Alisema kwa mwaka huu, wameboresha zawadi za washindi ili ziwe kivutio kwa washiriki wengi.

Edith amewataka washiriki wajitokeze kwa wingi, lakini timu tatu za wanaume na tatu za wanawake ndizo zitaingia hatua ya fainali kuu itakayofanyika Mwanza.

Alisema timu zitakazotwaa ubingwa mwaka huu kwa upande wa wanaume na wanawake, zitaingia fainali za mwakani kwa ajili ya kutetea ubingwa wao.

Naye, Meneja Masoko wa TBL, Fimbo Butallah, alitaja zawadi kuanzia ngazi ya mikoa, bingwa wa mkoa wanaume atapata sh. 800,000 na wanawake sh. 600,000 na fainali kuu bingwa wanaume ni sh. 2,600,000 na wanawake ni sh. 2,200,000, washindi wa pili kimkoa ni sh. 600,000 kwa wanaume na sh. 500,000 kwa wanawake na fainali kuu ni sh. 2,200,000 wanaume na sh. 1,600,000 wanawake.

Alisema washindi wa tatu kimkoa ni sh. 400,000 kwa wanaume na sh. 300,000 wanawake, fainali kuu ni sh. 1,600,000 kwa wanaume na wanawake ni sh. 850,000, wa nne kimkoa ni sh. 350,000 wanaume na wanawake ni sh. 250,000, na fainali kuu ni sh. 850,000 kwa wanaume, wakati wanawake itakuwa sh. 600,000.

Edith alisema washindi wa tano hadi 10 kimkoa, kila mmoja atapata sh. 200,000 kwa wanaume na sh. 150,000 kwa wanawake na katika fainali sh. 400,000 zitatolewa kwa wanaume na wanawake ni sh. 200,000.

No comments:

Post a Comment