11 October 2011
NHC yawageukia JWTZ wizara nyeti, polisi
*Yawapa miezi miwili la sivyo kutupwa nje
Na Willbroad Mathias
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limezidi kucharuka na sasa limezipa notisi ya
miezi miwili, Wizara nyeti na taasisi za serikali likiwemo Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuwa zimelipa limbikizo la madeni zinazodaiwa, vinginevyo litazipiga kufuli ofisi hizo.
Mbali na JWTZ, taasisi nyingine zinazodaiwa limbikizo la zaidi ya sh bilioni 2, ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Wizara ya Afya, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Jeshi la Polisi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ujenzi.
Wadaiwa wengine sugu ni Wakala wa Mjengo, Bodi ya Usajili wa Waandisi, Wizara ya Kilimo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Utamaduni, Katibu Mkuu Wizara ya Kazi Maendeleo ya Vijana.
Nyingine ni Idara ya Habari Maelezo, Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza, Tume ya Haki za Binadamu na Haki na Utawala Bora, Msajili wa Mahakama Kuu Tanga, Ofisi ya Rais, Tumre ya Utumishi wa Umma na Mkuu wa Jeshi la Polisi.
Taarifa hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Nehemiah Mchechu katika mkutano wake na waandishi wa habari alioitisha kuelezea oparesheni ya kuwabana wadaiwa sugu inayoendeshwa na shirika hilo nchi nzima.
Bw. Mchechu alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya wadaiwa hao kuomba muda wa mwezi mmoja ili kulipa madeni yao kabla ya kutolewa vifaa vyao nje, lakini kwa upande wao wakaona ili kuondoa lawama, bora wawaongezee mwezi mmoja.
"Hata hivyo, pamoja na kuomba mwezi mmoja, sisi tumeona tuwape miezi miwili na kama watashindwa, tutaanza oparesheni mpya ambayo ni kuzitia kufuli ofisi hizo huku utaratibu mwingine wa kisheria ukifuata," alisema Bw. Mchechu.
Wiki iliyopita shirika hilo limeshaanza kutekeleza dhamira yake kwa kutoa nje vifaa vya wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
"Kazi ya kuwatoa wapangaji wanaodaiwa kwenye nyumba ni gharama kubwa, kwa taasisi, mashirika ya umma na ofisi za serikali zinazodaiwa na shirika, tunatoa muda wa miezi miwili yaani Oktoba na Novemba 2012 kulipa malimbikizo wanayodaiwa na shirika," aliongeza Bw. Mchechu.
Alisema endapo malimbikizo hayo hayatalipwa ndani ya kipindi hicho, wataendelea na utaratibu wao mpya wa kuzifunga ofisi hizo.
Alisema endapo kama malipo hayatafanyika baada ya hatua hiyo kuchukuliwa, watawakabidhi madalali wa mahakama ambao watatoa notisi nyingine ya siku 14, ili waweze kulipa madeni yao kabla ya kukamata mali kwa ajili ya kupiga mnada kufidia madeni hayo.
"Huu ni utaratibu mpya ambao tunaamini kwamba ukitekelezwa utaleta tija kwa shirika, taasisi na mashirika ya umma yanayodaiwa," alisema.
Mkugenzi huyo alisema, kwa mujibu wa taarifa za mwenendo wa shirika, taasisi, mashirika ya umma na wizara zinadaiwa kiasi cha sh. bilioni 2.1.
Alisema kuwa kwa sasa shirika lina kazi kubwa ya ujenzi wa nyumba, hivyo linahitaji fedha hizo ili kazi itekelezwe kwa wakati.
"Tukumbuke kwamba athari iliyopo mbele yetu iwapo tutashindwa kukusanya madeni ni kushindwa mpango mkakati wa manufaa kwa wananachi wengi," alisema mkurugenzi huyo.
Alisitiza kuwa wapangaji wa shirika kutimiza ni wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati, pale inapobidi shirika litafuata taratibu zote za kisheria kuhakikisha kuwa wanakusanya madeni yote.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa anataka iweleweke kuwa nyumba za shirika ni mali ya Watanzania wote na kwamba uhalali wa mpangaji kuendelea kukaa katika nyumba utakuwepo tu kama atatekeleza wajibu wake wa kulipa kodi stahili kwa wakati.
Akizungumza kuhusu oparesheni hiyo, Bw. Mchechu alisema kuwa shirika hilo halina ugomvi na serikali kwa kuwa nalo ni sehemu ya serikali, isipokuwa linapambana na wateja wasiotimiza wajibu wao kama wapangaji kwa kutolipa kodi.
"Serikali ni kubwa sana na ni taasisi chache ambazo ni wapangaji wa NHC, na hizi taasisi zinapaswa kutambua wajibu wake kama wengine," alisema Bw. Mchechu.
Alisema, pamoja na kutambua utaratibu wa malipo kwa taasisi za umma kuchukua muda mrefu, lakini utaratibu wa kulipa kodi upo palepale kama ulivyo kwa wapangaji wengine wa shirika.
Bw. Mchechu alisema kabla oparesheni hiyo kuanza, serikali na taasisi zake ilishataarifiwa umuhimu wa kulipa kodi ya pango ambayo kimsingi hutengwa kwenye bajeti inayopitishwa na bunge.
"Baadhi ya taasisi na mashirika yamekuwa na malimbikizo ya zaidi hata ya miaka mitatu, huu ni uvumilivu wa shirika kwa serikali yake," alifafanua mkurugenzi huyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Hii kwa vyovyote ni aibu! Ni kwa nini wizara na idara za serikali pamoja na mashirika ya umma, watu ambao waanapewa hela kwa ajili hiyo kwenye baajeti zao washindwe/waache kulipa kodi ya pango? Huu ni mtazamo wa dharau ambao unatokana na kudharau mali ya umma.
ReplyDeleteSerikali kuun isiingilie iache NHC ishughulike. Sio busara kwa Mheshimiwa Rais kuliingilia shirika , badala yake awaite wahusika na kuwachukulia hatua.
Kama walitengewa hela hiyo kwenye bajeti waeleze wameipeleka wapi, na kama hawakuiweka kwenye bajeti waeleze kwa nini. Uzembe huu usiruhusiwe kuendelea na watu wasikingiwe kifua na mamlaka za juu. Kama watu binafsi wamekuwa wakifanyiwa hivyo na hawakupata msaada wowote kutoka kwenye serikali yao kwa nini hizi ofisi zilindwe?