12 October 2011

African Stars Band waibuka na Twanga Festival

Na Frank Balile

BENDI ya muziki ya African Stars 'Twanga Pepeta', imeandaa tamasha kubwa la Twanga Festival litakalohusisha sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika
Novemba 6, mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET), Asha Baraka, alisema tamasha hilo litajumuisha burudani mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu.

“Tumeangalia mambo mengi katika uandaaji wa tamasha hili, kutakuwa na burudani mbalimbali kuanzia asubuhi mpaka jioni, ikiwemo soka,” alisema.

Asha alisema tamasha hilo limepangwa kufanyika kwenye viwanja wa Leaders Club, Kinondoni Dar es Salaam, ambapo timu mbalimbali zitaanza kushindana Jumamosi kwenye viwanja hivyo.

Asha alisema timu 12 za soka za jijini Dar es Salaam, zitashiriki michuano hiyo iliyopewa jina la Veteran ASET Football Tournament, ambapo zimegawanywa katika makundi mawili, A na B.

Aliztaja timu zitakazoshiriki michuano hiyo maalum ni Brake Point, Mango Garden, Singasinga, Namanga, Kigamboni na Ukonga, zitakazokuwa Kundi A.

Kundi B litakuwa na timu za Twanga Pepeta FC, Taxi Driver, Mpilipili, BM FC, Leaders Club na Daladala Camp.

Mkurugenzi huyo wa ASET, alisema kuwa, fainali ya michuano ya soka itafanyika Novemba 6, siku ambayo tamasha hilo la Twanga Festival litakuwa likifanyika.

“Fainali ya mpira wa miguu tumepanga ichezwe siku ya ya tamasha letu, hivyo kutakuwa na shamrashamra kuanzia asubuhi kwenye viwanja wa Leaders Club,” alisema.

Asha alisema kabla ya kufanyika kwa tamasha hilo, wameandaa hafla ya utambulisho wa albamu mpya ya 11 ya bendi hiyo kwa wadau na waandishi wa habari itakayofanyika kwenye ukumbi wa Maisha Club, Oktoba 18, mwaka huu.

Alisema wametoa mwaliko kwa makampuni, taasisi za benki, vyombo vya habari, waigiza wa filamu, kampuni za simu za mkononi, Chama cha Hakimiliki (COSOTA), Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO's), ili waweze kuona kazi zinazofanywa na wasanii.

“Tumefanya hivyo makusudi ili wadau hao waweze kuona wasanii wanavyofanya kazi zao, lengo letu ni kushirikiana nao katika mambo mbalimbali,” alisema.

No comments:

Post a Comment