11 October 2011

Mbunge CCM ashtakiwa kwa kutishia kuua

*Wa CHADEMA nusura wafutiwe dhamana

Na Waandishi Wetu, Mbeya, Tabora

MBUNGE wa Jimbo la Mbarali (CCM), Bw. Modestus Kirufi amepandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Mkoa kujibu mashtaka ya kutishia kuua kwa
maneno na kisha kutupwa rumande hadi kesi yake itakapotajwa tena.

Akisoma mashtaka dhidi yake mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Bw. Michael Mtaite, Mwendesha Mashtaka Bw. Grifini Mwakapeje alisema kuwa mbunge huyo alitenda kosa hilo Machi 16, mwaka huu.

Aliieleza mahakama kuwa mbunge huyo alitishia kwa maneno kumuua Ofisa Mtendaji wa Kata ya Luiwa, Bw. Jordan Masweve kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Bw. Kirufi alikana kutoa vitisho hivyo na wakili anayemtetea, Bw. Mwakolo aliiomba mahakama hiyo kuruhusu dhamana kwa mteja wake hadi kesi hiyo itakapotajwa tena kwa kuwa ni haki yake kisheria.

Hakimu Bw. Mtaite alikataa ombi hilo na kutaka muda wa kutafakari masharti ya dhamana yaliyowekwa na hivyo kutaka mtuhumiwa kupelekwa mahabusu hadi Oktober 24, 2011 kesi hiyo itakapotajwa tena.

Bw. Kirufi anakuwa mbunge wa kwanza kwa wabunge wa CCM mkoani hapa kukamatwa na kufikishwa mahakamani, na wa pili baada ya mbunge wa Mbeya Mjini, Bw. Joseph Mbilinyi (CHADEMA) kushtakiwa kwa kufanya mkutano bila kibali cha polisi.

Wabunge Chadema nusra kufutiwa dhamana

Mahakama mkoani Tabora imewaonya na kutishia kufuta dhamana zao wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kushindwa kuhudhuria kesi yao ya kumdhalilisha Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Bi. Fatuma kimario.

Akitoa onyo hilo Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Bw. Thomas Simba alisema mahakama inalazimika kutoa onyo kwa washtakiwa hao kutokana na kutoridhika na sababu zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi.

Alisema kitendo hicho kinaoonesha kuwa washtakiwa hao wanajali kazi zao na kutotoa kipaumbele kwa mahakama, hivyo kama hawatafika mahakamani watafutiwa dhamana ili wakakae rumande.

Alihoji iwapo wasingepata dhamani wangewa wapi muda na ruhusa ya kuhudhuria vikao hivyo vya kamati.

Hakimu Simba alienda mbali zaidi na kusema hata kama ni wabunge wanatakiwa kuheshimu sheria za mahakama hivyo chochote kinachotokea kinatakiwa kutolewa kwa maelezo na sababu zinazosababisha kutokuhudhuria mahakamani, na kuomba ruhusa vinginevyo kesi hiyo haitaisha mapema.

Kabla ya uamuzi huo, Wakili Bw. Mussa Kwikima aliyewawakilisha washtakiwa hao mahakamani hapo aliiambia mahakama kuwa
washtakiwa wa kwanza na wa pili ambao ni wabunge, Bw. Sylivester Kasulumbai na Bi. Suzan Kiwanga wameshindwa kuhudhuria mahakamani kwa sababu wako kwenye vikao vya Kamati ya Bunge.

Wakili huyo alisema kwamba mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Bw. Anwar Kashaga ameshindwa kuhudhuria kwa vile yuko hospitalini Bugando jijini Mwanza akipatiwa matibabu, madai ambayo pia yalielezwa na mdhamini wa mshtakiwa huyo mahakamani hapo.

Licha yakutoa maelezo hayo aliomba radhi kwa wateja wake kwa kutofika mahakamni jana na kuhakikishia mahakama hiyo kwamba kosa kama hilo halitatokea tena katika kipindi kijacho cha usikilizwaji wa kesi hiyo,

Hoja hizo zilipingwa na mawakili wa upande wa mashtaka, Bw. Juma Masanja na Bw. Mugisha Mboneko ambao waliieleza mahakama kwamba hoja hizo hazitoshi kuifanya mahakama ikubaliane nao kwa sababu hazina vielelezo vyovyote kama inavyotakiwa kisheria.

Mshitakiwa wa nne katika kesi hiyo aliyeoongezwa katika mashtaka hayo Oktoba 4, mwaka huu, Bw. Robert William amerudishwa rumande baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana ya ahadi ya shilingi milioni 5, mali isiyohamishika na wadhamini wawili.

Akisoma mashtaka hayo, Mwendesha Mashtaka Bw. Juma Masanja akisaidiwa na Mugisha Mbonea alidai kuwa mnamo Septemba 15, mwaka huu majira ya mchana huko katika Kijiji cha Isakamaliwa wilaya Igunga, mshtakiwa wa kwanza, Bw. Kasulumbai alitoa lugha ya matusi kwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Bi. Fatuma Kimario.

Aliendelea kwamba mshtakiwa huyo alisema: "Malaya mkubwa, huyu ndiye niliyetaka kuzaa naye mpumbavu mkubwa, DC gani huyo hana akili?

Pia ilidaiwa kuwa huko katika Kijiji cha Isakamaliwa Wilaya ya Igunga washtakiwa kwa pamoja walimshambulia Bi. Kimario na kumsababishia maumivi ya kichwa.

Katika kosa la tatu washtakiwa hao wote kwa pamoja wanadaiwa kumshikilia Bi. Kimario bila uhalali na kinyume cha Sheria kifungu namba (253) kanuni ya adhabu sura namba 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kosa la nne wanalodaiwa kutenda watuhumiwa hao kumwibia Bi. Kimario dimu ya mkononi aina ya Samsung yenye thamani ya sh. 400,000.

Upande wa utetezi unaongozwa na mwanasheria wa chama hicho, Bw. Tundu Lisu akisaidiwa na wakili wa kujitegemea, Bw. Musa Kwikima. Wote walitimiza masharti ya dhamana na kuachiwa huru hadi leo.

Imeandikwa na Charles Mwakipesile, Mbeya; na Moses Mabula, Tabora

No comments:

Post a Comment