Na Mwandishi Wetu
MKUTANO Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), umepanga kufanyika Desemba 17, 2011, Dar es Salaam Zoo
mjini Dar es Salaam.
Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando, alisema Kamati ya Utendaji ya chama hicho iliyokutana hivi karibuni na kupanga mkutano huo ufanyike eneo hilo lililopo Kilometa 37 kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Alisema lengo la kuupeleka mkutano huo nje ya jiji, ni kuwaweka pamoja kwa siku nzima waandishi wa habari za michezo na kubadilishana mawazo kuhusu mambo mbalimbali yaliyotokea mwaka 2011.
“Nia ya TASWA ni kumaliza Mkutano Mkuu saa nane mchana na baada ya hapo, waandishi watajumuika katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam Zoo kwa nia ya kuburudika na kutumia nafasi hiyo kupongezana kwa kazi za mwaka 2011 na kupanga mikakati ya mwaka 2012,” alisema.
Kamati ya Utendaji, awali ilitaka mkutano huo ufanyike Desemba 31, Bagamoyo mkoani Pwani, ili kuukaribisha kwa pamoja mwaka mpya 2012, lakini wajumbe walikubaliana ufanyike Dar es Salaam Zoo Desemba 17, kwani Desemba 31 wengi hupenda kuukaribisha mwaka wakiwa na familia zao.
Mhando alisema kutokana na hali hiyo, TASWA inawaomba wanachama wake wajipange kwa ajili ya mkutano huo, ambao ajenda zake zitakuwa zile za kawaida zilizopo kwenye Katiba, ambazo ni pamoja na Ripoti ya Utendaji kwa mwaka 2010/2011, Ripoti ya Fedha 2010/2011.
Pia, wanachama ambao watapenda kuwa na ajenda nyingine ili zijadiliwe kwenye mkutano huo, wanatakiwa kuziwasilisha kwa maandishi kwa Katibu Mkuu wa TASWA ama Katibu Msaidizi wa TASWA, ambapo mwisho umepangwa kuwa 30 mwaka huu.
Katibu Mkuu huyo, alisema TASWA inawaomba wanachama wake wote kuhakikisha wanalipia ada za uanachama za mwaka 2011/2012 haraka kwa kuwasiliana na Mhazini wa TASWA, Sultani Sikilo ama Mhazini Msaidizi Mohammed Mkangara na mwisho utakuwa Desemba 10, mwaka huu.
“Wengi wa wanachama walilipa ada kabla ya uchaguzi uliopita, ambayo ilikuwa ya mwaka 2010/2011, hivyo wanatakiwa kulipa ya mwaka 2011/2012 ili waweze kuhudhuria mkutano wetu mkuu,” alisema.
Mhando alisema huo utakuwa Mkutano Mkuu wa Kwanza tangu uongozi wa TASWA chini ya Uenyekiti wa Juma Pinto uingie madarakani Agosti 15, mwaka jana.
Wakati huo huo, TASWA inawashukuru wote waliofanikisha mafunzo ya waandishi wa habari za michezo yaliyofanyika Oktoba 1 na 2 mwaka huu mkoani Morogoro na kushirikisha wadau 40.
Mhando aliishukuru TASWA Morogoro chini ya uenyekiti wa Nickson Mkilanya, kwa ushirikiano mkubwa uliowezesha kufanikisha mafunzo hayo.
Mbali na Mwenyekiti huyo, pia imewashukuru wadau wake mhariri mkongwe Said Salim, mdau Anna Kibira, mwanasheria Damas Ndumbaro, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera na Alfred Selengia ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya kuendeleza mpira wa wavu Tanzania, kwa mada zao walizotoa kwenye mafunzo hayo.
Katibu huyo aliishukuru kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania na Kampuni ya mabasi ya Al Saedy kwa kudhamini mafunzo hayo na kuwaomba waendelee na ushirikiano huo.
Mafunzo mengine, yatafanyika mkoani Arusha Novemba mwaka huu, hivyo wanawaomba wadau wa michezo kushirikiana na chama hicho kufanikisha mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment