11 October 2011

Askofu: Rasilimali zinufaishe wananchi

*Aonya kinyume chake ni kuhatarisha amani
*Ataka migodi ya kusini iepushe migogoro


Na Dennis Gondwe, Njombe

SERIKALI imeshauriwa kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinatumika kwa maslahi ya nchi na kuwanufaisha wananchi wenyewe walio wengi, vinginevyo ni
 kuhatarisha amani iliyopo.

Ushauri huo ulitolewa na Askofu Mteule wa Dayosisi ya Kusini- Njombe, Isaya Mengele katika ibada ya kumsimika uaskofu, na kumuingiza kazini msaidizi wa Askofu, Dkt. George Fihavango.

Ibada hiyo iliyoongozwa na Mkuu wa Kanisa la Kinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) nchini, Askofu Dkt. Alex Malasusa ilifanyika katika Kanisa Kuu, Dayosisi ya Kusini Njombe.
Askofu Mengele alisema kuwa rasilimali za nchi zinapogawanywa kwa maslahi ya nchi na wanufaikaji wakawa ni wananchi, nchi hutawaliwa kwa amani na utulivu.

Madini kusini na mazingira

Kiongozi huo alikwenda mbali zaidi na kutoa tahadhari kwa upande wa madini, akisema migodi itakayoanzishwa katika ukanda wa kusini mwa nchi, uanzishwaji, uratibu na usimamizi wake lazima uwe mzuri ili kuepusha migogoro inayoshuhudiwa katika ukanda wa kaskazini mwa nchi.

Akizungumzia uhifadhi wa mazingira, alisema kuwa ni muhimu kwa serikali na wadau wengine wote wa maendeleo na wenye mapenzi mema na nchi hii kutilia mkazo dhana ya uhifadhi wa mazingira ili kuinusuru nchi dhidi ya uharibifu wa mazingira ili nchi iwe mahali salama kwa ustawi wa binadamu.

Askofu huyo aliipongeza serikali katika jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo na kuisifu kutojiingiza katika masuala la kidini, hali inayochangia ukuaji na ustawi wa uhuru wa kuabudu unaoendana na misingi ya kidemokrasia nchini.

Akimsimika rasmi, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Askofu Alex Malasusa aliwataka viongozi wa dini kutokutumia nafasi zao kwa maslahi ya kisiasa.

Katika salamu za Mkoa wa Iringa, zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma, alimpongeza Askofu Mengele kwa uteuzi wake. Aidha, amewaomba viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla wao kukaa chini na kutafakari juu ya nchi na kuiombea ili iendelee kuwa na amani, upendo na utulivu.
Vile vile, Dkt. Ishengoma ililishukuru kanisa hilo kwa michango na ushiriki wake katika kuiletea maendeleo jamii. Aliitaja michango hiyo kuwa ni pamoja na kuijenga jamii katika maadili, kuwafanya wananchi wake kuwa wema na huduma za jamii kama elimu na afya.

2 comments:

  1. kiukweli baba Askofu amenena vema san na kwa upnande wangu mimi ninampa bigi up

    ReplyDelete
  2. aache kujihusisha na uchawi, kama mwenzake......, maana na yeye anatuhumia kama vile ambavyo.......anatuhumiwa kumbaka mtoto wa askofu mwenzie tumaini

    ReplyDelete