Rais Jakaya Kikwete akiongoza kikao maalumu cha wadau wa sekta ya nishati nchini kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana. |
Na Mwandishi Maalumu
RAIS Jakaya Kikwete amewataka watendaji wa serikali yake kutambua kuwa nchi iko katika hali ya
dharura kubwa ya upatikanaji wa nishati ya umeme, na hivyo wafanye maamuzi ya haraka, bila kigugumizi, kukabiliana na hali hiyo kwa manufaa ya wananchi.
“Tuko katika hali ya dharura na mimi sioni hisia za uharaka wa kuchukua maamuzi na hatua nyingine muhimu za kukabiliana na udharura wa upatikanaji wa umeme na nyenzo nyingi za kuzalisha umeme.
Hatuwezi kuendeleza kuwa na kigugumizi katika kuchukua maamuzi ya kuitoa nchi katika changamoto kubwa hizi za upatikanaji wa nishati,” Rais Kikwete aliwaambia watendaji hao wa serikali yake wanaohusiana na sekta ya nishati.
“Ubwana mkubwa wa kila mmoja wetu utatambuliwa kutokana na mafanikio ambayo kila mmoja wetu ataonesha katika kuchangia katika kukabiliana na hali hii ya upatikanaji wa nishati,” alisema Rais Kikwete katika kikao cha watendaji hao kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam jana.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza katika kikao alichokiitisha kuzungumzia ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na upatikanaji wa gesi asilia nchini kwa ajili ya kuzalisha umeme ambao umekuwa katika mgawo nchini tangu Novemba mwaka jana kutokana na ukame ulioathiri kina cha maji katika mabwawa yote ya kuzalisha umeme nchini.
Hali hiyo, imeilazimisha nchi kuchukua hatua nyingi za kupatikana kwa umeme wa dharura mbali na hatua ambazo tayari Serikali ya Rais Kikwete ilikuwa imeanza kuchukua kuongeza kasi ya upatikanaji wa umeme kutokana na vyanzo vingine mbali na maji.
Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho cha kazi ni pamoja na Waziri wa Fedha, Bw. Mustafa Mkulo, Waziri wa Sheria na Katiba, Bi. Celina Kombani, Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Phillemoni Luhanjo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema, na maofisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Benki Kuu ya Tanzania, Tume ya Mipango, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Kikao hicho kimejadili, miongoni mwa mambo mengine, ujenzi wa bomba kubwa zaidi la kusafirisha gesi asilia kutoka Mikoa ya Mtwara na Lindi hadi Dar es salaam linalokusudiwa kujengwa na serikali ili kuongeza kasi ya upatikanaji gesi kwa ajili ya matumizi ya kuzalishaji umeme na matumizi ya viwandani katika sehemu mbalimbali za nchi, badala ya bomba la sasa ambalo ni dogo zaidi.
No comments:
Post a Comment