*Yawapandisha vijana nane
Na Zahoro Mlanzi
TIMU ya Simba, imeamua kujichimbia katika fukwe za Bamba Beach, Kigamboni kwa ajili ya kujinoa kwa michezo yao ya Ligi Kuu Bara, huku ikiwa na
mkakati wa kuhakikisha inashinda mechi zao tano zilizobaki.
Mbali na hilo, timu hiyo pia imewapandisha vijana wao sita kutoka katika timu yao ya vijana wenye miaka chini ya 20, kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kikosi cha wakubwa ambacho kinaonekana kuwa na majeruhi wengi.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi wa timu hiyo, Ibrahim Masoud 'Maestro', alisema timu hiyo ilianza kujifua katika fukwe hizo juzi jioni, baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Azam FC uliopigwa asubuhi.
"Timu imepiga kambi Bamba Beach ikijifua ili kuhakikisha tunaendeleza rekodi ya kutofungwa katika mechi za ligi, na kama unavyojua tuna operesheni ya kuhakikisha tunashinda mechi zetu tano zilizobaki katika mzunguko huu," alisema Maestro.
Alisema wachezaji kipa Juma Kaseja, Nassor Said 'Chollo' na Juma Nyosso waliokuwa katika kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars), walitarajiwa kujiunga na timu hiyo jana jioni, huku hali ya Victor Costa na Mwinyi Kazimoto, zikiendelea kuimarika taratibu.
Alisema mara baada ya kumalizika kwa mchezo wao wa Jumatatu wa vijana dhidi ya timu ya vijana ya Azam FC, ambao walishinda mabao 3-0, wameamua kuwapandisha wachezaji sita katika kikosi cha timu ya wakubwa.
Aliwataja wachezaji waliopandishwa ni kipa Abuu, Miraji Kadenge, Frank Sekule, Abdallah Seseme, Ramadhani Suzan na Ramadhani Abdallah, ambapo wana imani wataongeza nguvu katika kikosi chao.
Alisema timu yao ina vijana wenye vipaji vya hali ya juu na ndio maana hivi sasa wameamua kuwapa nafasi ili miaka ijayo, wawe na timu inayoaminika itakayofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
"Kama ungekuwepo katika mchezo dhidi ya Azam, haya ambayo nimekwambia ungeyaona, kama tutafanikiwa kuviweka pamoja hivi vipaji vya hawa vijana kwa asilimia kubwa, tutapata mafanikio makubwa na kuitangaza Simba zaidi," alisema Maestro.
Simba kwa sasa imeenguliwa kutoka kileleni na JKT Oljoro ambayo ina pointi 19, na kuwa nafasi ya pili kwa kujikusanyia pointi 18, huku ikiwa na michezo miwili mkononi, JKT Ruvu ikifuatia katika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 15, sawa na Azam na Mtibwa kwa pointi, lakini zikitofautina kwa mabao.
Timu hiyo inatarajia kucheza na African Lyon Oktoba 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mfululizo wa michezo ya ligi hiyo.
No comments:
Post a Comment