23 August 2011

Msekwa aja juu kuhusu tuhuma za kuuza viwanja

Na Pendo Mtibuche, Dodoma

MWENYEKITI wa Bodi ya Hifadhi ya Ngorongoro, Bw. Pius Msekwa amekanusha vikali tuhuma za kugawa maeneo ya kujenga hoteli za kitalii kwa wawekezaji na
kusema maneno hayo ni ya
kutaka kumchonganisha yeye na wakuu wake.

Bw. Msekwa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara
alisema kuwa maneno yaliyosemwa na Mbunge Kaika Telele wakati akichangia Bajeti ya
Wizara ya Maliasili na Utalii yalilenga kuchafua jina lake kwa umma.

Alisema kuwa maneno hayo yalikuwa ni maneno ya kashfa kwake na yalijikita kuchafua historia ya muda mrefu ya uadilifu wake katika kutekeleza kazi za umma alizopangiwa katika nyakati mbalimbali na marais kuanzia rais Julius Nyerere hadi Rais Kikwete.

Akifafanua zaidi alisema kuwa akiwa ni Spika mstaafu wa Bunge anafahamu kwamba sheria ya haki na madaraka ya Bunge inatoa haki na uhuru wa kuchangia mawazo yao bungeni.

Alisema kuwa ibara ya 100 ya Katiba  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema
kwamba uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote au katika mahakama au
mahali pengine popote nje ya Bunge.

“Lakini ninafahamu wazi kwamba haki na uhuru huo haujumulishi haki au uhuru wa kusema uwongo bungeni ndiyo sababu kanuni za bunge  zina kifungu kinachopiga marufuku mbunge kusema uwongo bungeni  hali hii inakuwa vibaya zaidi kusema uongo dhidi ya mtu ambaye siyo mbunge kwa hiyo hawezi kujitetea ndani ya bunge,” alisema.

Bw. Msekwa ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge alisema hajui kama kuna kanuni inayomruhusu mtu ambaye si mbunge kuwasilisha malalamiko yake kwa Spika kutokana na kuzushiwa uongo ili ajitete na kusema kuwa kama kanuni hiyo ipo basi kinachofuata baada ya kukanusha madai ya mbunge huyo ni kutafuta kanuni hiyo na kujitetea kwa spika juu ya jambo analotuhumiwa.

Hata hivyo alisema kuwa tuhuma ya mbunge huyo dhidi yake ya kusema kuwa mwenyekiti
huyo wa Bodi hakuhudhuria mjadala wa Bunge wakati bajeti ya Wizara ya Maliasili na
Utalii ilipokuwa inawasilishwa  imetokana na dhana mpya iliyokuwa imejengeka ya kukusanya watu wengi Dodoma tena kwa gharama kubwa zaidi.

Bw. Msekwa alisema kuwa yeye kama mwenyekiti wa Bodi alikwishahudhuria kikao cha Kamati
ya Bunge inayoshughulika Maliasili na vile vile alikwishahudhuria kikao cha Kamati  ya Bunge inayoshughulikia Hesabu za Mashirika ya Umma Ngorongoro ikiwa ni Shirika la Umma.

“Katika kamati hiyo nilipewa nafasi ya kutoa maelezo pamoja na kujibu maswali ya
wabunge kuhusu usimamizi unaofanywa na Bodi yangu juu ya shughuli za mamlaka  ya
Ngorongoro,” alisema.

Akizungumzia maeneo ya ujenzi wa hoteli katika hifadhi hiyo alisema ujenzi wa hoteli katika hifadhi hiyo ulitangazwa kwa
wawekezaji kupitia magazeti yanayochapishwa hapa nchini katika matoleo yake ya Novemba 9 mwaka 2006 na baadaye vikao vya bodi vilishughulikia suala hilo.

Alisema kuwa ugawaji wa maeneo hayo ulifanyika kwa vikao maalum vilivyofanyika mwaka
2007 na hata mbunge huyo Telele alihudhuria mikutano hiyo  wakati huo akiwa mjumbe
wa Bodi  ya Ngorongoro.

Akizungumzia kashfa ya kutumia jina la Rais Jakaya Kikwete katika ugawaji viwanja mahali ambapo hairuhusiwi kujengwa hoteli Msekwa alisema kuwa maneno hayo ni ya uongo.


1 comment:

  1. Huu ni utamaduni wa viongozi wa Tanzania kila wanapo tuhumiwa na jambo fulani huwa wakali na kukanusha kila jambo.hawana utamduni wa kukubali jambo na kujirekesha na mifano ya viongozi wa namna hii ipo mingi sana.Wengi hukanusha madai yao alafu mwisho wa siku wanaamua kujiuzulu na wengine hukataa kabisa hata kujiuzulu kwa sababu za kunogewa na madaraka.Huwa wanalewa kabisa na uongozi.

    ReplyDelete