20 June 2012

Asamoah apewa 'last chance' Kagame Cup *Nizar aanza kazi, Kiiza naye ndani


Na Zahoro Mlanzi

WAKATI mshambuliaji kutoka Zambia, Davies Mwape akioneshwa mlango wa kutokea timu ya Yanga, imempa nafasi ya mwisho Mghana Kenneth Asamoah kuonesha makali yake katika michuano ya Kombe la Kagame la sivyo naye watamuacha.

Mbali na hilo, kiungo mpya wa timu hiyo, Nizar Khalfan jana alianza rasmi kibarua cha kuitumikia timu hiyo kwa kufanya mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake zaidi ya 17 waliokuwepo katika mazoezi hayo.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo kwenye Uwanja wa Kaunda, Dar es Salaam jana Kocha Msaidizi wa timu hiyo Fredy Felix 'Minziro', alisema Asamoah imeamuliwa abaki kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame lakini Mwape tayari ameshamalizana kila kitu na uongozi.

"Ni kweli Mwape licha ya kwamba unamuona mazoezi lakini hatutakuwa naye kwa msimu ujao, tayari uongozi umeshamalizana naye na hata Asamoah, naye anaangaliwa katika Kombe la Kagame na kama akiendelea kuonesha kiwango kile kile naye tutafikiria cha kufanya," alisema Minziro.

Alisema wachezaji hao wanalipwa fedha nyingi, hivyo walipaswa kuonesha kiwango tofauti na wachezaji wazawa ambapo kwa Mwape alishindwa kufanya hivyo, ndiyo maana wakaamua kusitisha mkataba wake ila Asamoah watamuangalia katika michuano hiyo.

"Unajua ukiwa mshambuliaji ni lazima ufunge tu huna jinsi na usipofunga mashabiki hawatakuelewa, Mwape katika mechi na Zamaleki ndiyo iliyomuweka pabaya kwa kupoteza nafasi nyingi za wazi," alisema Minziro.

Akizungumzia maandalizi kwa ujumla, Minziro alisema kwa sasa anawajenga wachezaji wake kuwa na stemina, ambapo baada ya wiki moja ataendelea na programu nyingine.

Wakati huohuo, Nizar ameanza rasmi mazoezi na timu hiyo ambapo mashabiki waliojitokeza katika mazoezi hayo walionesha kufurahishwa na uamuzi wake wa kujiunga na timu yao, ambapo kila alipogusa mpira walimshangilia.

Wachezaji ambao jana walikuwepo mazoezini ni kipa Yaw Berko, Godfrey Taita, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Canavaro', Ibrahim Job, Athuman Idd 'Chuji', Hamis Kiiza, Stephano Mwasika, Jeryson Tegete, Idrisa Rajab, Juma Seif 'Kijiko', Pius Kisambale, Asamoah, Omega Seme, Salum Telela na wengine watatu wa timu yao ya vijana.

No comments:

Post a Comment