11 July 2011

Yanga bingwa Kagame Cup

*Kazimoto akimbizwa hospitali

Na Zahoro Mlanzi

YANGA jana ilitawazwa kuwa mabingwa Kagame Castle Cup, baada ya kuwafunga watani wao jadi Simba bao 1-0 katika mechi ya fainali ya michuano hiyo
iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Bao la Yanga lilipatikana dakika ya 110 kupitia kwa Keneth Asamaoh, aliyeingia badala ya Jerry Tegete kwa kichwa akiunganisha krosi kutoka wingi ya kushoto.

Kwa matokeo hayo Yanga, ilikabidhiwa kombe la michuano hiyo, medali za dhahabu na kuzoa kitita dola 30,000 huku Simba ikishika nafasi ya pili na kukabidhiwa medali za fedha na kitita cha dola 20,000.

Katika mechi hiyo Simba ilianza kwa kasi na kufanya shambulizi la nguvu langoni mwa Yanga dakika ya tatu, lakini hata washambuliaji wake Haruna Moshi 'Boban' na Ulimboka Mwakingwe walishindwa kupenyeza mpira nyavuni.

Yanga ilijibu shambulizi hilo dakika ya saba, lakini Nadir Haroub 'Canavaro' aliunganisha vibaya kona iliyochongwa na Oscar Joshua.

Dakika ya 17 kiungo wa Simba, Mwinyikazi Moto alilazimika kutolewa nje kwa machela na kukimbizwa hospitali baada ya kuchezewa vibaya na Juma Seif 'Kijiko', ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Mohamed Banka.

Kutoka kwa kiungo huyo ilikuwa pigo kwa Simba, ambayo ilianza kupoteana sehemu ya kiungo na kuwaruhusu Yanga kujipanga vyema.

Yanga ilikosa tena bao la wazi dakika ya 23 baada ya Hamis Kiiza kuchezewa faulo Shija Mkina, lakini Tegete aliunganisha fyongo shuti la Joshua na mpira kutoka nje.

Kipindi cha pili Yanga iliingia kwa nguvu kutaka kupata bao lakini dakika ya 60, Tegete alishindwa kufunga baada ya kukutana na mpira uliopishwa na Davies Mwape kutokana krosi ya Godfrey Taita.

Baada ya kosa kosa hizo timu zote zilipunguza mashambulizi na kucheza kwa kutegeana.

Dakika ya 76, Kiiza alifunga mpira kwa kichwa hata hivyo lilikataliwa na mwamuzi kwa madai kwamba ya kufunga alikuwa ameotea.

Kuanzia dakika ya 80, wachezaji wote walionekana kuchoka lakini Yanga iliweza kuwabana wapinzani wao na kufanya mashambulizi mfululizo ambayo hayakuweza kuzaa bao.

Mwamuzi wa mchezo huo alilazimika kuongeza dakika 30, za ziada baada ya dakika 90 za kawaida timu hizo kushindwa kufungana.

Katika dakika za ziada, wachezaji wa Simba walionekana kuchoka na kuwapa nafasi Yanga kufanya mashambulizi ya mfululizo hadi walipopata bao hilo laushindi.

3 comments:

  1. Mhariri,
    Muwe mnaandika habari iliyokamilika. Nilitegemea mungeandika kinagaubaga suala la kukatika umeme Uwanja wa Taifa kwani ile ni "aibu ya Karne".

    Wakati ikijulikana kwamba umeme wa nchi hii ni mgogoro, hivi kweli imeshindikana kununua "Standby Generator???" Mapato yanayopatikana uwanjani hapo yanapelekwa wapi badala ya kuangalia kwanza vitu muhimu kama jenerata!!!

    Hebu angalia Mhe. Waziri wa Michezo alivyokuwa akihangaika kupiga simu ingalao tu kwa wakati ule umeme upatikane. Au tuseme ni hujuma!! Ikumbukwe kwamba mashindano yale yalikuwa yanaangaliwa katika Afrika yote kama si Duniani kote.

    Hivi kwa hali ile mtaweza au mtakuwa na nguvu za kuutangaza uwanja wetu nje ya nchi kwa mechi mbalimbali za kimataifa???

    Nadhani kwa kitendo kile, Meneja Mkuu wa uwanja inabidi ajiuzulu!!!

    ReplyDelete
  2. Swali la kujiuliza ni kwa nini Tanesco wazime umeme katika eneo hilo hali wakijua kwamba kulikuwa na maelfu ya watu uwanjani jambo ambalo lingeweza kusababisha madhara makubwa? Kwa kutambua umuhimu wa shughul iliyokuwa inafanyika pale kwa nchi yetu, Tanesco kwa nini hawakuondoa line hiyo kwenye mgawo? Na kwa nini umeme ukatike mara tu baada ya Simba kupata zawadi zao? Hii ni hujuma ya makusudi kuingiza utendaji kwenye ushabiki. Aliyefanya hivyo atambue hakuikomoa Yanga tu bali ameaibisha Taifa zima

    ReplyDelete
  3. Hapa kilichoelezewa na mwandishi wa habari hii ni matokeo ya mchezo huo. Suala la umeme kukatika halikuongelewa hapa, hivyo tuwe waelewa wa kile kichoandikwa.

    ReplyDelete