11 July 2011

Twiga Stars yatua na shaba yao

Na Zahoro Mlanzi

TIMU ya taifa ya wanawake 'Twiga Stars', inatarajia kutua nchini leo asubuhi ikitokea Zimbabwe ilipokwenda kushiriki mashindano ya nchi zilizo Kusini mwa
Afrika, ambapo ilishika nafasi ya tatu na kutwaa medali ya shaba.

Twiga Stars katika mashindano hayo yaliyoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA), ilishiriki kama timu mwalikwa pamoja na Malawi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema timu hiyo itatua Dar es Salaam saa 3.20 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways na baadaye saa 5 asubuhi wachezaji na Kocha, Charles Mkwasa watazungumza na vyombo vya habari.

"Mkwasa pamoja na benchi lake la ufundi watazungumzia mashindano hayo kwa ujumla wake na changamoto walizokutana nazo tangu walipoanza kucheza hatua ya makundi mpaka kutwaa ushindi wa tatu," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Alisema ana imani kwa matokeo hayo waliyoyapata itawasaidia katika maandalizi yao ya kujiandaa na Michezo ya Afrika itakayofanyika Maputo, Msumbiji Septemba mwaka huu.

Twiga Stars ilitwaa medali hiyo baada ya kuifunga Malawi mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Rufiro, Harare Zimbabwe ambapo mabao ya washindi yalifungwa na Asha Rashid 'Mwalala' aliyefunga mabao mawili na Mwanahamis Omari.

Mashindano hayo yalishirikisha timu nane kutoka katika ukanda huo ambazo ni Lesotho, Botswana, Afrika Kusini, Zambia, Msumbiji, Malawi na wenyeji Zimbabwe.

1 comment:

  1. Twiga stars wanastahili pongezi,wamekua wakitutoa kimasomaso kila wanapocheza nje ya nchi tofauti na timu tunazo zishabikia sijui simba na yanga,

    Hawa ni watoto yatima lakini wanauwezo hata ukiangalia mpira wao they are good!! big-up Mkwasa

    ReplyDelete