19 July 2011

SPUTANZA yazishukia Simba, Yanga

Na Addolph Bruno

CHAMA cha Wachezaji wa Mpira wa Miguu Tanzania (SPUTANZA), kimesema kimesikitishwa na tabia za klabu za soka nchini, zikiwemo Simba na Yanga kuwatoa wachezaji wao
kwa mkopo kwa klabu nyingine bila wenyewe kuridhia.

Akizungumza kwa masikitiko Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Saidi George, alisema chama hicho kinapinga hali hiyo kutokana na kwamba, inawakatisha tamaa wachezaji wanaochipukia.

Hivi karibuni klabu ya Simba imewatoa kwa mkopo wachezaji wake, Mussa Hassan 'Mgosi' na Mohamed Banka katika klabu ya Villa Squad, Juma Jabu (Moro United), Meshack Abel (African Lion),  ambapo baadhi yao akiwemo Banka na Jabu wamepinga ofa hizo wakidai kuwa, hawakushirikishwa.

Kwa upande wa Yanga, imewatoa wachezaji Salumu Telela kwenda Moro United, Beki Mganda Ton Ndollo kwenda Toto African na Omega Same na Idi Mbaga.

"Sina ukakika na klabu nyingine kuhusu kufanya hivyo, ila hali hiyo kwa kweli sio nzuri na tunaziomba klabu zibadilike, mchezaji anatakiwa kupewe taarifa na aone atafaidika vipi kimaslahi," alisema katibu huyo.

"Uhamisho wa wachezaji unapofanyika tena kwa mkopo au kwa namna nyingine,sio vyema kuficha na kumshtukiza mchezaji, kwanza anaumia kisaikolojia kwa sababu wengi wa wachezaji wetu, soka ndio kazi yao," alisema.

Katibu huyo alisema chama hicho kimejaribu kufanya mawasiliano na Baraza la Vyama Vya Michezo Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), kupitia kwa katibu wake Nicholas Musonye wakati wa mashindano ya Kombe la Kagame kuipitia na kuijadili upya sheria ya uhamisho wa wachezaji, lakini hakikufanikiwa.

"Hatujakata tamaa, tutaendelea kupigania haki za wachezaji wetu ambao ni wanachama wetu ili tuone soka letu linasonga mbele, wenzetu Ulaya wanafuata sana sheria katika uhamisho wa wachezaji, iwe kwa mikopo au vinginevyo, lakini sisi tunadharau," alisema.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimetoa wito kwa wachezaji kuona umuhimu wa kujiunga na SPUTANZA ili waweze kucheza soka wakiwa huru na kuepuka matatizo kama hayo.

No comments:

Post a Comment