Na Waandishi Wetu
KESI ya kupinga serikali kulipa sh. bilioni 94 kwa kampuni ya Dowans imeanza kunguruma katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam jana huku ikielezwa
kuwa kelele za nje haziisumbui mahakama hiyo kuendelea kuisikiliza.
Kesi hiyo imefunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na mashirika mengine 16 ya wanaharakati ikiwa na lengo la kupinga hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) iliyotolewa na Novemba 15, mwaka jana ikiliamuru Shirika la Umeme nchini (TANESCO) iilipe Dowans fidia ya sh bilioni 94 kwa kuvunja mkataba baina yake na kampuni hiyo kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Mahakama hiyo, Gerald Aksen akisaidia na wasuluhishi, Swithin Munyantwali na Jonathan Parker.
Januari 25, mwaka huu Dowans iliwasilisha Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam maombi ya usajili wa tuzo yake hiyo kupitia kwa Wakili Kenedy Fungamtama, ili ulipwaji wa fidia yake hiyo ufanyike kwa mujibu wa taratibu, kitendo ambacho kinapingwa na wanaharakati, wakisema ni kinyume cha sheria.
Kesi hiyo jana ilitajwa ili kuangalia kama pande zote husika zimepatiwa nyaraka zote husika, na kubainika hazikuwa zimewafikia wote
mujibu wa sheria na taratibu za uendeshaji kesi, hivyo mahakama iliziagiza kupeana nyaraka hiyo.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju aliiomba mahakama kuu impatie siku 21 kujiandaa kwa ajili ya kujibu hoja zinazohusiana na kesi hiyo, huku Dkt. Mvungi akiomba siku saba kujiandaa baada ya hapo, kama kutakuwa na kitu chochote cha kujibu katika hoja hizo zitakazowasilishwa na upande wa serikali.
LHRC kwa niaba ya mashirika hayo wamewasilisha pingamizi lenye hoja saba kupitia Kampuni ya Uwakili ya South Law Chambers Advocates mbele ya Jaji Emilly Mushi.
Kwanza, wanadai kuwa hawakuridhika na tuzo hiyo iliyotolewa na ICC kwa Dowans kwani TANESCO ni shirika la umma linalomilikiwa na Serikali ya Tanzania na fedha zinazoiendesha zinatokana na Watanzania walipa kodi.
Katika hoja ya pili wanadai kuwa hakuna mkataba wa kisheria uliofungwa baina ya TANESCO na Kampuni ya Dowans uliosababisha kuwepo kwa mgogoro ulioilazimu ICC kutoa tuzo hiyo kwa kampuni hiyo.
Sambamba na hoja hiyo, wanaharakati hao wameambatanisha na mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Richmond ambao Dowans iliurithi, unaodaiwa kuwa na mashaka kisheria, kama kielelezo.
Tatu, wanadai kuwa chini ya sheria za Tanzania, mkataba na tuzo hiyo kwa Dowans ni batili na umejaa dosari za kisheria.
Nne, wanaharakati hao wanadai kuwa chini ya sheria za Tanzania, Kampuni ya Richmond haikuwa na nguvu ya kisheria kuingia mkataba na Serikali ya Tanzania au na TANESCO, huku wakiambatanisha na kielelezo cha taarifa ya matokeo ya uchunguzi wa Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza uhalali wake.
Tano wameeleza kuwa kutokuwepo kwa mkataba hai kati ya Richmond na TANESCO, jukumu hilo lilitakiwa kutekelezwa na wajibu pingamizi wa kwanza na wa pili, ambalo ndilo lilisababisha kutolewa kwa tuzo hiyo kuwa batili, na hivyo tuzo iliyotolewa na ICC haiwezi kukubaliwa wala kutekelezwa na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Katika hoja ya sita ya pingamizi hilo, wanaharakati hao wanadai kuwa tuzo hiyo ilitolewa hata kabla ya mgogoro mwingine kutatuliwa katika mahakama nyingine ya Houston nchini Marekani, baina ya Richmond na Dowans Tanzania Limited juu ya umiliki wa mashine za kuzalishia umeme, ambazo zinahusiana na tuzo hiyo.
Katika hoja ya saba ya pingamizi hilo, wanaharakati hao wanadai kuwa maombi ya usajili wa tuzo iliyotolewa na ICC ambayo yamewasilishwa Mahakama Kuu hayapaswi kukubaliwa kwa kuwa imetokana na mkataba batili baina ya Richmond na TANESCO.
Kesi hiyo itaendelea tena Machi 30, mwaka huu, Jaji Mushi ataangalia kama taratibu na maamuzi aliyoyatoa yamezingatiwa na pande husika kama alivyoagiza.
Watanzania kwa kukosa kazi kama Mtikila tumekithiri!!!!
ReplyDeleteyaan wewe mtoa maona namba moja unaona hilo ni kukosa kazi!! watu wanakaa kutete maslahi ya taifa unaona ni kukosa kazi!! kweli ukiwa na roho ya kifisadi uchungu kwa taifa unayeyuka. kaa chini ufikiri kwa kina nd utoe maoni yako!
ReplyDelete