Na Tumaini Makene
UTAFITI wa Taasisi za Ifakara Health Institute (IHI) na Venture Strategies Innovations (VSI), umebaini uwezekano wa kupunguza vifo vya akina mama, hususan vile
vinavyosababishwa na kutokwa damu nyingi mara baada ya kujifungua, kwa teknolojia rahisi, kuliko inayotumika sasa.
Katika mapendekezo ya utafiti huo, taasisi hiyo imeshauri kuwa vifo hivyo vinadhibitika kwa akina mama wajawazito kwa kupatiwa vidonge vya dawa iitwayo Misoprostol, wakati wa kujifungua, hata kama mama mjamzito atajifungulia sehemu isiyokuwa na huduma za afya, mathalani nyumbani.
Akiwasilisha sehemu ya matokeo ya utafiti huo uliofanyika katika Wilaya nne za Rufiji, Ulanga, Kilombero na Kigoma Mjini, mmoja wa watafiti, Bi. Ndola Prata alisema kuwa dawa ya Misoprostol ni muhimu kwa sasa kwa kuwa utaratibu wa sasa wa kuzuia utokaji wa damu kwa wingi baada ya kujifungua unakabiliwa na changamoto nyingi.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na dawa zilizopo kutumia sindano ambayo inaathiriwa na mwanga na joto, zinahitaji mjamzito ajifungulie akiwa katika sehemu rasmi zinapotolewa huduma za afya na pia zinahitaji wataalam wa afya kutumika.
Changomoto hizo zinasababisha ugumu katika upatikanaji wake, hivyo ni wanawake wachache wanaoweza kumudu kupata huduma hiyo ya kuzuia utokwaji damu nyingi baada ya kujifungua.
Badala yake alisema dawa ya misoprostol ni rahisi kwa sababu ziko katika namna ya vidonge, ambako dozi moja pekee huhitajika. Pia ni salama kutumika hata kama mzazi akijifungulia nyumbani, ambapo hazihitaji wataalam wa afya, kwa kuwa hata wakunga wa jadi au mama mjamzito mwenyewe wanaweza, baada ya kupata maelekezo.
Alisema kutokana na juhudi za pamoja kati ya VSI na Wizara ya Afya, zilisaidia dawa hiyo kupata usajili nchini kwa ajili ya matumizi hayo ya kuzuia utokaji wa damu nyingi tangu mwaka 2007, huku pia ikisajiliwa katika orodha ya taifa ya madawa muhimu, mwaka huo huo.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa IHI, Dkt. Godfrey Mbaruku alisema kuwa kwa mujibu wa takwimu, takribani wanawake 340,000 wanakufa kila mwaka duniani kote kutokana na matatizo wakati wa ujauzito na kujifungua, ambapo asilimia 99 ya vifo hivyo vinatokea katika nchi maskini.
Kwa upande wa Tanzania, alisema kuwa maelfu ya wanawake wanakufa kila mwaka kutokana na matatizo ya uzazi, hasa wakati wa kujifungua, ambapo kwa kila saa moja anakufa mwanamke mmoja.
Alizitaja sababu zinazochangia matatizo ya utokaji mwingi wa damu kwa akina mama baada ya kujifungua kuwa ni pamoja na maambukizo, shinikizo la damu, kazi ngumu pamoja na utoaji wa mimba.
"Mapendekezo yetu katika utafiti ni pamoja na usambazaji wa dawa hii ya misoprostol unapaswa kuboreshwa ili zifike nchi nzima kuhakikisha maisha ya wanawake wengi yananusuriwa dhidi ya tishio hili wakati wa kujifungua.
"Pia kunahitajika kuwepo mafunzo zaidi kwa watoaji huduma za afya ili kusambaza dawa hizi, juhudi hizo zinapaswa kwenda sanjali na utoaji elimu pia kwa umma kuhusu matumizi ya misoprostol," alisema Dkt. Mbaruku.
No comments:
Post a Comment