*Yainyuka Kagera Sugar 1-0
Na Theonista Juma, Kagera
BAO pekee lililofungwa na mshambuliaji raia wa Zambia, Davies Mwape katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya
Kagera Sugar limeifanya Yanga kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Mchezo huo uliopigwa jana katika Uwanja wa Kaitaba mjini hapa, umeifanya Yanga kuongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 35 na kuishusha Simba ambayo imebaki na pointi zake 34 ikiwa na mchezo mmoja mkononi na Azam FC ikiwa nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 32.
Katika mchezo huo, wenyeji Kagera ndiyo waliokuwa wa kwanza kubisha hodi langoni mwa Yanga dakika ya pili kupitia kwa Godfrey Taita, aliyepiga krosi safi iliyoshindwa kumaliziwa na Benjamin Asukile.
Yanga ilijipanga na kufanya shambulizi la nguvu dakika ya saba na kuzaa matunda kwa bao lililofungwa na Mwape baada ya kuunasa mpira uliorudishwa vibaya na beki, David Charles na kukwamisha mpira wavuni, bao hilo ni la sita kwa mchezaji huyo katika ligi hiyo.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na dakika ya 33, nusura Jeryson Tegete aifungie Yanga bao la pili baada ya kushindwa kuunganisha krosi ya Kigi Makasi akiwa amebaki na kipa.
Baada ya kushambuliwa mfululizo Kagera, ilifanya mabadiliko ambapo iliwatoa George Katila na Daud Jumanne na kuingia Sunday Frank na Paul Ngwai, ambao waliiongezea uhai timu hiyo.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Kagera, ikionesha dhahiri kutaka kusawazisha bao hilo ambapo dakika ya 60, Steven Mazanda alipiga 'tick tack' iliyodakwa na Kipa Yaw Berko akiunganisha krosi ya Taita.
Kagera iliendelea kuliandama lango la Yanga na dakika ya 65, Gaudance Mwaikimba alikosa bao la wazi akibaki na kipa Berko kwa kupiga shuti lililopanguliwa na mabeki kuondosha hatari.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu ambapo kama si washambuliaji wa Kagera kushikwa na kigugumizi kila waliporikaribia lango la Yanga, ingeweza kusawazisha bao hilo kwani kipindi hicho ilitengeneza nafasi nyingi.
No comments:
Post a Comment