Na Addolph Bruno
BAADA ya kuibanjua mabao 3-0 African Lyon, katika mchezo wa juzi na kuzikaba koo Simba na Yanga katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara
Azam FC, imesema wataendelea kukaza buti katika michezo iliyobaki ili wajiweke katika mazingira mazuri.
Azam ambayo kabla ya mchezo huo ilikuwa nyuma ya Yanga kwa pointi 29, sasa ina pointi 32 sawa na Yanga lakini ikiwa ya pili katika msimamo wa ligi kwa kuwa na uwiano mzuri wa mabao huku Simba ikiongoza ikiwa na pointi 34 kabla ya Yanga kucheza jana na Kagera Sugar.
Akizungumza Dar es salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Idrisa Nassor alisema wameupokea ushindi huo kwa furaha, ingawa bado wana kazi ngumu mbele yao katika ligi hiyo inayoendelea.
"Hatuwezi kuchukulia kama tumeshinda, ninachoweza kusema tuna faraja lakini hatuna budi kucheza kwa nguvu zaidi kwa sababu bado tuna kazi kubwa ya kuendelea kufanya vyema," alisema.
Alisema kutokana na ushindi huo wa juzi, wataitumia nafasi hiyo kuchuana na vinara wa ligi hiyo, Simba na Yanga ili waweze kuunyakua ubingwa wa Tanzania Bara unaoshikiliwa na Simba.
Nassor alisema sasa wanafanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mchezo mwingine dhidi ya Majimaji utakaopigwa machi 2, mwaka huu katika uwanja wa Mkwakwani Tanga.
No comments:
Post a Comment