18 February 2011

Lipumba ataka uchunguzi huru Gongolamboto

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetoa taarifa ya kusikitishwa na tukio la milipuko ya mabomu ambalo ni la pili kutokea katika kambi za Jeshi la Wananchi na
kuomba uchunguzi huru wa tukio hilo.

Kimeitaka serikali kuwaomba nchi marafiki wa kijeshi na zile ambako silaha hizo zilinunuliwa kutoa msaada wa watalaamu kufanya uchunguzi ili kubainisha sababu ya kulipuka wakati muda wake wa matumizi haujaisha.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema milipuko hiyo imesababisha mtafaruku mkubwa kwa wakazi wa maeneo ya jirani na kambi hiyo, ambapo mamia ya wakazi hao wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani na kuweka kambi za muda maeneo ya kambi ya kikosi cha kutuliza ghasia, Uwanja wa Taifa, vituo vya polisi kama Buguruni na wengi wao kuhifadhiwa kwa ndugu na jamaa.

"Tukio hili linachukua taswira ya tukio la Jumapili ya Aprili 29  mwaka 2009, ambapo, milipuko ya mabomu ilitokea katika ghala la kuhifadhia mabomu katika kikosi cha 671 KJ, Mbagala na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 20 na wengine wengi kupata ulemavu wa maisha, pamoja na uharibifu mkubwa wa majengo na maeneo ya makazi," alisema Profesa Lpumba.

Alisema pamoja na ahadi mbalimbali kutoka kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi ya kuhakikisha kuwa tukio kama hilo halitatokea, tayari tukio kubwa zaidi ya lile la Mbagala limetokea.

Alisema waziri huyo alionesha ukaidi pale alipotakiwa kujiuzulu kutokana na uzembe uliofanyika ndani ya wizara yake, ya kushindwa kuweka mazingira salama yasiyoweza kuleta madhara kwa wananchi.

"CUF tunahuzunishwa na uzembe huu unaoendelea kujitokeza kwa makusudi na kuonesha dharau ya kutothamini uhai wa raia wa nchi hii ambapo dhamana ya jeshi la Ulinzi ni kulinda mipaka ya nchi na raia wake," alisema Profesa Lipumba.

Alisema chama chake kwa mara nyingine kinamtaka Dkt. Mwinyi na Mkuu wa JWTZ, Jenerali Davis Mwamunyange kuwajibika kwa kujiuzulu mara moja kutokana na ukaidi na kushindwa kudhibiti madhara yaliyojitokeza siku za nyuma.

"Tunamsihi Waziri Mwinyi kulinda heshima yake kwa kufuata nyayo za baba yake Mzee Ali Hassan Mwinyi alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alipojiuzulu kutokana sakata la mauaji mkoani Shinyanga," alisema Profesa Lipumba.

Alisisitiza kuwa matukio hao yanasababisha maafa yakiwemo, kupoteza nguvu kazi ya taifa (ambayo ni vifo), kupoteza uwezo kuzalisha kutokana na ulemavu wanaoupata na kusababisha kuwa tegemezi.

Alisema hali hiyo inaliingizia taifa hasara ya ununuzi wa vifaa vingine mbadala vya kijeshi ya vilivyoangamia pasipo matumizi stahiki, jamii husika iliyoathiriwa kupoteza mali zao na kuchanganyikiwa kisaikolojia hadi kufikia kushindwa kumudu maisha.

"CUF tunaungana na Watanzania wote kwa msiba huu mzito wa kitaifa na kuwapa pole familia, ndugu na jamaa za wananchi waliopoteza maisha yao kutokana na milipuko ya mabomu hayo na kuwataka wawe na subira katika kipindi hiki cha majonzi, na kumuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi," alisema.

Alisma CUF inamtaka Rais Jakaya Kikwete kuwahakikishia wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuishi bila hofu kutokana na matukio yanayoendelea kujitokeza ya milipuko katika kambi za jeshi, ili hali jiji likiwa limezungukwa na kambi mbalimbali za jeshi katika kila upande, Kigamboni, Lugalo, Mgulani, Upanga, Mabibo, Mbweni na kwengineko.

2 comments:

  1. HUYO KIKWETE MWENYEWE NI MWANAJESHI UNAJUAJE KAMA NDIO KAWATUMA? PIGENI KELELE LAKINI WATANZANIA TUNAISHA NA MABOMU HAPO NDIO BADO MPAKA TUTEKETEE. RAIS HANA UCHUNGU WOWOTE WALA MKUU WA MAJESHI KAMA ANGEKUFA AU KUUMIA RIDHIWANI ANGECHANGAMKIA HARAKA LAKINI NYIE WA GONGOLAMBOTO ETI NDIO MMEKUTA KAMBI ZA JESHI HIVYO VIFO MMEVITAFUTA. EE MUNGU PELEKA MIAKA HII MITANO HARAKA HUYU MKWERE AENDE TUMECHOKA. WENZETU LIBYA LEO WAMEANZA MAMBO

    ReplyDelete
  2. Kikwete, waziri Mwinyi, Waziri Nahodha na mkuu wa JWTZ wawajibike sasa imetosha. Serikali inauwa watu lakini hakuna haijali wala kujifunza maana haioni makosa. Watu walikufa Mbagala kwa mabomu, Arusha kwa risasi za moto na sasa Gongolamboto kwa mabomu, lakini tunadanganyiwa Tume itaundwa kuchunguza ambayo mwisho wa siku hakuna tutakachosikia. Hivi watanzania tumekuwa watu wa kudanganywa mpaka lini? Raisi wa Tunisia, Misri walikuwa waongo hivihivi mwishowake wananchi walisimamama kidete mitaani kuwakataa. Nawaomba watanzania wenzangu popote mlipo tujipange mitaani kwa amani bila fujo tumkatae Kikwete maana amezidi uongo kwa watanzania. Yote aliyoahidi 2005 kama si machache hakuna alichofanya. Ajila kwa vijana hakuna, umeme hakuna, vitu bei juu, uchaguzi umepita sasa machinga wanasumbuliwa, mapato nao wamekuwa mbogo. atanzania msingojee muujiza, tumkatae Kikwete aondoke madarakani.

    ReplyDelete