18 February 2011

Watu 20 wathibitika kufa 184 kujeruhiwa

Na Waandishi Wetu

WATU 20 wamekufa na wengine 184 kujeruhiwa kutokana na milipuko ya mabomu iliyotokea kwenye maghala ya kuhifadhia silaha katika kambi ya
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Gongolamboto jijiji Dar es Salaam juzi siku.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Dar es Salaam nchini, Mrakibu Msaidizi (ASP) Advera Senso aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa miili ya waliokufa imehifadhiwa katika hospitali za Amana, Muhimbili na Temeke.

Awali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema bungeni kuwa idadi ya watu waliokufa ilikuwa 17 na kuwa milipuko ya mabomu hayo ilisababisha madhara makubwa ya majeruhi, watoto wadogo kupotea na uharibifu mkubwa wa mali.

Bi. Senso alisema wahanga wa tukuio hilo wamepewa hifadhi ya muda katika uwanja wa mpira wa Uhuru, Viwanja vya Maonesho ya Sabasaba, Kituo cha Polisi Tazara, Buguruni na Msimbazi.

Aliwataka watu waliopotelewa na ndugu kufika katika vituo hivyo ili kuwatambua.

"Jeshi la polisi linapenda kuwasisitiza wananchi kuwa watulivu na kuendelea na kazi zao kama kawaida kwa sababu hali hiyo tayari imedhibitiwa kwa sasa (jana mchana) na kusingekuwa na milipuko inayoendelea," alisisitiza Bi. Senso.

Alitoa mwito kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapona kitu ambacho si cha kawaida katika maeneo yao kupitia namba  0774-039029, 0782-114515, 0782-60334 na 0755-756410.

No comments:

Post a Comment