18 February 2011

Kambi ya Upinzani: Mwinyi, Mwamunyange wajiuzulu

* Yataka maghala ya silaha yahamishwe maeneo ya raia

Na Reuben Kagaruki

KAMBI ya Upinzani Bungeni imeeleza kushtushwa na taarifa za milipuko ya mabomu katika ghala la silaha la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na
imeshauri Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange kuwajibika kwa kujiuzulu nyadhifa zao.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga wa kambi hiyo, Bw. Joseph Selasini alieleza jana katika taarifa ya kambi hiyo kuwa viongozi hao wanatakiwa kuwajibika kutokana na milipuko ya mabomu iliyotokea Gongolamboto, jijini Dar es Salaam, juzi usiku.

Bw. Selasini alisema; "Dkt. Hussein Mwinyi alikuwa Waziri wa Ulinzi wakati wa maafa ya Mbagala na Jenerali Mwamunyange alikuwa Mkuu wa Majeshi. Maafa ya Mbagala yalitokea chini ya dhamana na au usimamizi wao. Na mara baada ya maafa hayo, Waziri Mwinyi na Jenerali Mwamunyange waliahidi taifa kwamba maafa ya aina hii hayatatokea tena. Sasa yametokea," alisema na kuongeza;

"Ahadi yao ilikuwa sio ya kweli, viongozi hawa hawana budi kuwajibika kwa hiari yao wenyewe au kuwajibishwa kama itahitajika."

Bw. Selasini aliongeza kusema kwamba hadi leo hakuna taarifa yoyote rasmi iliyowahi kutolewa hadharani kwa wananchi au kwa wawakilishi wao bungeni juu ya chanzo cha maafa hayo.

Kambi hiyo imewapa pole ndugu, jamaa na wananchi wote wa Tanzania kutokana na maafa yaliyosababishwa na mabomu hayo.

"Mamlaka zote za umma zinazohusika zichukue hatua za haraka kuhakikisha wananchi wote walioathirika na maafa hayo wanapatiwa huduma zote wanazohitaji katika kipindi hiki," alisema Bw. Selasini.

Alisema ni muhimu kwa vyombo vya usalama kuhakikisha ulinzi wa mali za wananchi katika maeneo yote yaliyoathirika ikiwa ni pamoja na kuwapatia matibabu.

Taarifa ya kambi ya upinzani ilieleza kuwa tukio hilo ni la kushtusha na kusikitisha hasa kwa kuzingatia kuwa haijapita miaka miwili tangu tukio la aina hiyo litokee Mbagala, Dar es Salaam.

Tukio hilo lilisababisha vifo vya zaidi ya watu 30 na uharibifu wa mali.

"Milipuko ya Gongo la Mboto inaonesha dhahiri kuwa Serikali ya Awamu Nne ya CCM haijajifunza lolote kutokana na maafa yaliyotokea Mbagala mwaka juzi," alisema Bw. Selasini na kuongeza;

"Kama Serikali ingejifunza kutokana na maafa hayo ingeshachukua hatua za dharura na za haraka kuhakikisha maafa ya aina hiyo hayatokei tena."

Bw.Selasini alishauri maghala yote ya silaha na mabomu yaliyo karibu na maeneo wanayoishi raia nayahamishwe maeneo wanayokaa raia.

Kambi hiyo imependekeza iundwe tume huru ya uchunguzi au kamati teule ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuchunguza kwa kina chanzo cha milipuko ya Gongo la Mboto.

Kaimu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Bw. Tundu Lissu alisisitiza hoja hiyo akihoji kama viongozi hao walijifunza kitu ni hatua gani walizichukua ili kudhibiti hali hiyo.

Hata hivyo alisema ubovu wa masuala ya kisera na kiutawala ndiyo yanayosababisha kuwepo kwa matukio kama hayo hali ambapo alihoji kwa nini maeneo kama hayo ya kutunzia silaha yawekwe katika maeneo ya makazi ya watu.

Kutokana na hali hiyo alisema ni wakati mwafaka sasa kwa Waziri wa Ulinzi na Mkuu wa Majeshi wajiuzulu au waachie nyadhifa zao kwani inaonesha wazi kuwa katika usimamizi wao wa masuala ya kijeshi kuwa nchi haiko salama.

15 comments:

  1. Nadhani wapinzani hamna subra,badala ya kukaa na kufariji walioumia na kutafakari tayari mnatafuta umaarufu humo,mabomu yametokea jana usiku,hamjajua chanzo chake,tayari mmekurupuka,nadhani mnaomba maafa yatokee ili mlaumu serikali watu wawaone mnafanya kazi, Ningefurahishwa kama mngezikataa Sh 90,000,000/= mlizopewa kununua magari zitumike kuhamisha hayo maghala ya silaha. Saa mnapopewa rushwa na serikali kama hiyo na nyingine mnakaa kimya lakini janga likitokea tu mbio kwenye vyombo vya habari utafikiri mlikaa kuombea litokee

    ReplyDelete
  2. Ni lazima Mwinyi na Mwamunyange wajihuzuru nyadhifa zao.Tusibabaishe mambo kabisa.Mambo ya siasa juu ya jambo hili hayahusiki hakuna CHADEMA,CCM wala CUF.Cha msingi raia wawe na mshikamano kuwaondoa madarakani Mwinyi pamoja na mwamunyange.

    ReplyDelete
  3. Hakuna haja ya subira, watu wamekufa, kuna haja ya subira tena? Baada ya mabomu ya Mbagala kuua watu, tulifanya subira sasa hivi hatudanganyiki. Na wewe unataka subira gani? Unataka mpaka yaripuke mengine kule Kigamboni na kuua tena?

    ReplyDelete
  4. mtangulizi wa maoni inaonesha huna akili nzuri, na hujui kufikiri kwa kina. msemaji ameshaonesha masikitiko yake na vielelezo vya kwa nini tukio kama hili, linatokea tena mara ya tatu mfululizo bila utekeleza wa kuzuia lisitokee.
    anapoieleza serikali na wahusika wajiuzulu haina maana hajali maafa, hata mimi nisiye wa chadema siungi mkono ujinga kama wa mtangulizi wa maoni.
    nakubaliana viongozi wahusika wajiuzulu kuonyesha masikitiko ya uzembe wao au watendaji wao kwa sababu, viongozi hao ndio walitakiwa wawe wa kwanza kutafuta mbini mbadala baada ya tukio la maafa ya awali Gongola mboto huko huko, mbagala na tena gongo lamboto.
    nadhani msemaji wa awali ni mbumbu wa kufikiri ambaye ni sawa na mzazi ambaye mtoto wake kikojozi anapoharibu godoro, hafikirii wazo la kukomesha tabia itakayomgharimu magodoro, harufu na afya ya mtoto.
    nina imani si kila wazo la wapinzani ni baya, yapo mengine mazuri sana, ila kwa uzembe na ujinga, tunayakataa.
    Juzi wametuambia (serikali kupitia polisi) tunaua watu tukakataa, baada ya siku moja mungu akathibitisha maneno yao kwa wawili kifo cha mbarali tukakanusha; bado mungu anaendele kuthibitisha kwamba; serikali inaua watu kwa uzembe wake wa kutowajibika na kutoa haki.
    wahenga kila siku wanasema mshahara wa dhambi ni mauti, uchakachuaji na wizi wa kura ni mauti ya wananchi.kubalini kosa na kuomba msamaha kwa kuwadharirisha wachungaji na mashehe waliokemea tabia ya mauaji na kuwaomba msamah; hali itakuwa swali.

    ReplyDelete
  5. eng. mwakapango, E.P.AFebruary 18, 2011 at 3:33 PM

    kuna mambo ya kusubiri lakini siyo hayo yanayosababisha watanzania kupoteza maisha yao. hata hivyo hiyo ndiyo kazi kubwa ya serikali kivuli. mmechukua hatua stahili ya kuishauri serikali JK apime mwenyewe na atoe uamuzi utaomsaidia yeye ili kuepukana na matukio ya namna hii.

    ReplyDelete
  6. Mchangiaji wa kwanza unataka subira. saafi saaana.

    Maneno yako ya kutaka pawe na subira yangekuwa na maana zaidi kama mmoja wa ndugu zako angekuwa ni mmoja wa waliokufa, ingefaa zaidi yakukute wewe mwenyewe kisha utwambie kuwa tuwe na subira hapo tungekuelewa.

    Watu wamekufa kwa uzembe kisha unasema tuwe na subira ya nini? Hili si jambo jipya maana miaka miwili iliyopita yalilipuka Mbagala, sasa hata MAKABURI hatujajengea yanalipuka Gongolamboto, na Viongozi ni walewale, wala hawashtuki!, hawaoni kama ni tatizo, na kama wataendelea kubakia madarakani tutazamie milipuko mingine itakayouwa Watanzania wengine wengi tu, maana kati yao hakuna anayeonesha kujali na kuzuia ajali za namna hii zisitokee. Hata Baba yake Hussein, Mzee Mwinyi alishaonesha mfano kwa kujiuzulu nafasi yake ya Uwaziri wa mambo ya ndani pale yalipotokea mauaji ya watu Mkoani Shinyanga, alionesha ujasiri na kuwajibika kama Kiongozi. Nawe Mwana fuata nyayo za BABAKO,JIUZULU japo ni ngumu kuachia ulaji!

    Viongozi wetu wengi leo hawapo tayari kuwajibika kwa makosa yao na au makosa yanayofanywa na wasaidizi wao, Tumemuona Hosea, Mwanyika,Meghji, Idrisa( EPA, IPTL, KAGODA, MWANANCHI, MEREMETA, NEC, IGP, RICHMOND, DOWANS, RTC, NDC, NMC, NASACO, TICTS, BODI YA PAMBA, BODI YA SUKARI, BODI YA KAHAWA, RADA, ATC, TIPPER, TRC, KAMATA, UDA, TAZARA NTC, NK) na wengi wengineo na wakati mwingine hata mamlaka zilizo juu yao zimeshindwa kuwawajibisha maana WANAKULA NAO. MAMBO YA KULINDANA!

    ReplyDelete
  7. Wote mliotoa maoni kumpinga aliyetoa maoni ya mwanzo inaelekea akili zenu mbovu,huyo jamaa kasema wabunge hao wa upinzani wangekataa mailioni ya mapesa waliogawana juzi,kila mbunge million 90 za kununulia magari ili zihamishe maghala ya silaha mbona hilo hamlisemei.wapumbavu wakubwa nyie,watu wanagawana pesa huko bungeni za kununulia magari,hamlioni hilo,mnalalamikia ajali,kulipuka kwa maghala hata huko Ulaya huwa yanalipuka tu. nyie ni wapumbavu sana hao wabunge wenu wanaishi maisha ya peponi wewe unashindia mlo mmoja unaishia kuandika kwenye mitandao mambo ya hovyo

    ReplyDelete
  8. Mtu akijamba pia mtamwambia ajiuzulu,mabomu ni ajali kweli,inaweza ikatokea wakati wowote tu,nashangaa wanaowaambia wataalam wa jeshi wekeni air condition,mnashangaza sana kila mtu anajifanya anajua,mngekuwa wajuzi hivyo nchi ingeoza hii?

    ReplyDelete
  9. Sitegemei kama Tanzani kuna watu uelewa wao ni mdogo kiasi hicho. Hivi mtu unapotetea uzembe kama huu uliogharimu damu za watu ni kitu gani basi utakachosema viongozi wajuzuru. Tunawajeshi wengi wazuri, tunaviongozi wengi wazuri watachukua nyazifa zao, Mkuu wa Majeshi na Waziri wa Ulinzi siyo miungu. Richimondi haikumwaga damu ila viongozi wakubwa kabisa 3 walijiuzuru. Leo tuendelee kucheka na na hawa waliomwaga damu ya Watanzania wenzetu. Tushikamane ili viongozi wawajibike. Wahusika lazima wawajibike. Naomba watu mnaotoa hoja mkitetea yaliyotokea mkumbuke kuwa si mara ya kwanza, yalitokea kwanza mbagara, sasa utaniambie hii ni bahati mbaya basi Duniani hakuna uzembe.

    ReplyDelete
  10. Wewe ndugu unayetukana watoa maoni kuwa ni wapumbavu wakubwa basi mungu akusamehe kwa kuwa hujui utendalo. Sitaki kukurudishia matusi yako lakini naomba uwe na nidhamu na pia lugha nzuri unapotoa maoni yako hata kama hayakupendezi tuwe na tabia ya kuvumiliana. Kwa kuwatetea viongozi wa serikali katika hili ni udumavu wa akili na inaonyesha mtu wa namna hiyo ana maslahi ya karibu na Viongozi hao wazembe. Swala la kulinganisha maafa ya Gongo la Mboto na mil, 90 za wabunge ni kukosa mweleko na hoja. Please get informed that pesa hizo wabunge wamekopeshwa na watalipa kupitia mishahara na posho zao. Ni sawa na wanafunzi wanaokopeshwa sasa useme wasikopeshwe eti fedha zihamishe maghala ya silaha kwani hakuna fedha zingine za kufanya kazi hiyo? Mbona juzi pinda ametemba kuwa wanakusanya bil 400 kila mwezi zinakwenda wapi? Wewe jamaa mchangiaji uache kufikiri kifisadi inaonyesha hao mafisadi wa serikali ya Tanzania ni baba zako au mama zako. Ipo siku tutawatafuta na kuvichoma vibenki vyenu mnavyoanzisha kutokana na kuiba fedha za watanzania. Kumbuka Kaka wa Mke wa Rais aliyefukuzwa huko Tunisia alikuwa na benki kubwa iliyotokana na wizi wa dada yake akiwa ikulu na juzi waandamanaji wameichoma moto. Suala la Mwinyi na Mwamunyange kuachia ngazi halina mjadala na wanapaswa wafanye hivyo au Kikwete awafukuze kazi haraka na kuweka wengine watakaolinda watanzania. Nawaunga mkono viongozi wa upinzani kushinikiza hilo na kazi yao nikulishikia bango mpaka wang'oke ama Rais alazimishwe kuwang'oa. Mbona Lowassa alijihudhuru kwa kosa ambalo hakulifanya iweje hawa waliotuahidi katika tukio la awali kuwa halitatokea tena jingine washindwe kujiuzulu. Ili serikali ipate heshima kwa wananchi wake hawa wasisubiri maandamano bali wawahi wenyewe kuchia ngazi. Kuwatetea hawa ni kutetea muaji yaendelee kwani inaonyesha silaha hizo za kivita zimekwisha muda wake na zinastahili kuteketezwa lakini jeshi wataalamu wake hawajui hilo. Mbona jeshi la leo si la akina Mwita Kyaro hili lina wasomi iweje mambo haya yatokee kama sio uzembe wa mkuu wa majeshi.
    WAZIRI NA MKUU WA MAJESHI ONYESHENI KUKERWA NA JAMBO HILI KWA KUACHIA NGAZI NYIE WENYEWE MTAPATA HESHIMA

    ReplyDelete
  11. Inaonesha JWTZ wanapuuza sana sera ya Afya, Usalama na Mazingira (HSE) katika maeneo yao.

    Wawajibishwe mara moja na lazime iwepo accountability kwa yeyote aliezembea kazi yake.

    Kuna silaha zimeteketea lakini pia inawezekana huu ulikuwa mpango wa baadhi ya wahujumu kuiba silaha hizo kwa matumizi ya kihalifu na hata ya kihaini! Don't leave any stone...!

    Roho za raia zimepotea, mali zao pia. Serikali, kwa upande wake, lazima IFIDIE hasara hii na ikiwezekana mahakama zitumike kuwapa fundisho watendaji waliozembea.

    Tathmini ifanywe kuangalia usalama wa ghala zote za silaha nchini zilizo karibu na maeneo ya wanachi.

    ReplyDelete
  12. Inakuwaje wakati kama huu, mkuu wa nchi anacheka cheka, video inayoonyesha kamanda wa jeshi akitoa taaraifa ya mambo yaliotokea kwa wakuu wake inamwonyesha Rais ambayo pia ni amiri jeshi mkuu akichekacheka, Pia nimeona kwenye picha ya watu wa Voda wakitangaza kuanza kwa kampeini yao ya kusaidia watu wa maafa Mwamvita Makamba ndio meno yote nje kabisa. Hawa Kikwete na Makamba wanajua nini ambacho wananchi hatujakijua.
    KWa kweli inasikitisha jinsi viongozi wanavyoliendesha hili taifa, Kwanza rushwa bila uoga (Richmond, Madini, Kiwira, Dowans,Kagoda na nyingine nyingi), Elimu inaporomoka (ona matokeo ya kidato cha nne, na jinsi watawala wanavyoshindwa kuelewana na wanafunzi wa vyuo vikuu amabao ndio wataalamu wetu wa kesho), Milipuko ya mabomu (Kwanza gongolamboto, alafu mbagala, sasa tena gongolamboto), Ukosefu wa umeme( Ni miaka hamsini tangu tumepata uhuru kutoka kwa mkoroni). Jamani, yaani hii orosha ya hayo mapungufu yaani haina mwisho. Ni lini watanzania tutaanza kuwajibika, au kuwawajibisha hawa viongozi ambao wanatakiwa kuwa wanafanya kazi kwa maslahi ya taifa(wananchi)

    ReplyDelete
  13. Ebwana hata mimi nimeziona hizo, nilidhani niko peke yangu kumbe wadau pia mmegundua, hihi kweli inanitia mashaka zaidi.
    Jionee mwenyewe
    Video Link:
    http://www.youtube.com/watch?v=j4G7oribxDY

    Picha ya Voda
    Link:http://issamichuzi.blogspot.com/2011/02/vodacom-foundation-kusaidia-wahanga-wa.html

    ReplyDelete
  14. Ni vigumu kuamini kwamba huyu ndugu wa kwanza kuchangia anatumia mfumo wa ubongo kufikiri. Kuna dalili zote kwamba anatumia kiungo kingine kabisa kufanya hivyo, na bila shaka ni tumbo.
    Mchangiaji haonyeshi uchungu hata chembe! naana adiriki kuleta mizaha ya eti shilingi milioni 90 walizokopeshwa wabunge. Sijui alitaka wapinzani wazisuse ili tena iwe ishu? Sera ya kulipa marupurupu yanayolipwa sasa bungeni ni ya CCM na kila chama kilichoweka mgombea wake wa urais katika uchaguzi uliopita kilikuwa na sera zake na hatimaye CCM ndiyo "Iliyoshinda" ndiyo kusema wapinzani itawabidi kufuata sera zilizopigiwa kura na wananchi (Kama ni kweli wananchi waliichagua CCM).
    Turudi kwenye mada; kujiuzulu kwa Mwinyi, Mwamunyange ni muhimu kupisha uchunguzi huru, wa haki na wazi. Izingatiwe kwamba hili ni tukio la pili ndani ya miaka mitatu, na hakuna kilichofanywa cha maana baada ya tukio la awali ambapo pia mali na maisha ya wananchi zilipotea. Katika nchi zenye ufanisi katika uwajibikaji hata Waziri Mkuu angejiuzulu ingawa kwetu hapa hizo ni ndoto!
    Kwa vyovyote vile yako maswali mengi ya kujibu kuliko maelezo "Cheap" ya Shimbo na wazembe wenzake ya ati "Mabomu yaliisha muda wake".
    Shimbo na "wasemaji" wake wazingatie kwamba kuna watu wengi tu uraiani wenye ujuzi wa juu kabisa wa mabomu na milipuko,kwa hiyo wanapotoa taarifa za namna ile kwa umma, wapo wanaozipima kauli zao kwa mapana na kuziponda kauli zao zinapoonekana kukosa ukweli.

    ReplyDelete
  15. Ni jambo la kusikitisha kusikia kuhusu kifo cha mtu hata kama ni mmoja iwe kwa ajali au kwa dhamira ya binadamu mwingine. Kinachonishangaza mimi ni namna watu wanavyotoa maoni yao. Yapo maoni ya watu ninayoweza kuoyapokea kama fundisho kwangu katika maisha na mengine nisiyaweke maanani. Lugha ya matusi imetawala sana sasa katika utoaji wa maoni. Naihesabu lugha hii kama ya mitaani. Swala la kulipuka kwa mabomu Gongo la Mboto na vifo vya watu na kuharibika kwa mali zao si jambo la kawaida iwe kwa ajili au kwa makusudi na uzembe wa mtu au watu. Ni kweli ya kwamba watu wamekufa. Je tunapofiwa na kwenda mazishini watu huwa basi hawaongei wala kucheka? Mbona kwanye misiba hata bao huwa linachezwa na wengine hata karata? Kuna makabila mengine hutengeneza hata vileo na kucheza ngoma msibani. Kama hii ilikuwa ni ajali iliyotokea bila uzembe wa mtu sioni sababu ya kuwalaumu viongozi wa nchi. JK ni binadamu kama wewe na wala si Mungu akilala ajue ya kwamba kesho itatokea ajali mto Wami. Je gari lake lilipozima njiani mara mbili na kutolewa kuingia jengine ilikuwaje? Alipoanguka jukwaani ilikuwaje? Si binadamu tu kama mimi na wewe? Ninachokiomba ni kwamba tunapotoa ushauri basi hekima na busara zitumike ili kuwasaidia wale tuliowachagua na kuwakabidhi uongozi watuongoze ipasavyo. Na tukiona hawakubali basi uchazi ujao tusiwachague.POLENI WANA G`MBOTO MWENYEZI MAULANA MUNGU WA REHEMA AWAFARIJI.

    ReplyDelete