Na Addolph Bruno
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro imetangaza wasanii watakaoshiriki tuzo za Kilimanjaro 'Kilimanjaro Music Awards'
mwaka 2011 katika kategori 22.
Fainali za tuzo hizo, ambazo hufanyika kila mwaka kwa zinatarajiwa kutolewa Machi 26, mwaka huu Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja wa bia hiyo, George Kavishe alisema wasanii hao wameteuliwa kwa ustadi mkubwa na kampuni ya Innovex iliyobobea katika fani hiyo, baada ya kuyafanyia kazi kwa umakini maombi ya wadau wa muziki waliyokuwa wakituma.
Alisema wasanii walioteuliwa wamegawanywa katika makundi ambayo yanahusisha majina matano, mpaka sita ya wasanii wanaowania tuzo mbalimbali zikiwemo za Msanii Bora wa Kike wa Muziki na Msanii wa Bora Muziki wa Kiume.
Wengine ni Mwimbaji Bora wa Kiume, Mwimbaji Bora wa Kike, Wimbo Bora wa Taarabu, Wimbo Bora wa mwaka na Wimbo Bora wa Kiswahili wa Bendi na Msanii mpya anayechipukia.
Kavishe alisema tuzo hizo pia zitashirikisha wasanii watano kutoka nchi za Afrika Mashariki, ambao watashindania tuzo ya wimbo bora ya mwaka kupitia nyimbo zao.
Nyimbo zitakazoshindaniwa na wasanii hao ni Nitafanya wa Kidumu akishirikiana na Lady Jay Dee, Kare wa kundi la P-Unit, Songambele wa Alfa wa Rwanda akishirikiana na AY, Vuvuzela wa GoodLife na Kasepiki wa Bebe Cool wa Uganda.
Aliwataja baadhi ya wasanii walioteuliwa ni pamoja na Linah, Shaa, Mwasiti, Khadija Kopa na Lady Jay D wanaowania tuzo za msanii bora wa kike ambapo tuzo za msanii bora wa kiume zinawaniwa na Abass Kianzi '20%', Ali Kiba, Barnaba, Belle 9, Banana Zoro pamoja na Diamond.
Wengine ni Gelly wa Rymes anayewania tuzo ya wimbo bora wa mwaka kupitia kibao chake cha Mama Ntilie, Sam wa Ukweli na kibao cha Sina Raha, pamoja na Chegge na wimbo wa Mkono Mmoja, huku tuzo za mtayarishaji bora wa mwaka zikiwaniwa na Marco Chali, Lamar, Man Water, Bob Junior na Pancho Latino.
No comments:
Post a Comment