22 February 2011

BFT kuwapa semina makocha wa ngumi

Na Mwali Ibrahim

SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), linatarajia kutoa semina kwa makocha wote wa timu zitakazoshiriki mashindano ya taifa ya
Klabu Bingwa Februari 25, Dar es Salaam.

Mashindano hayo, yanatarajia kufanyika Februari 26 hadi Machi 5 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo timu 21 zimethibitisha kushiriki.

Akizungumza Dar es Salaam jana Msemaji wa BFT, Eckland Mwaffisi alisema watatoa semina hiyo elekezi kwa makocha hao, ili kuwaweka tayari kwa ajili ya mashindano hayo.

Alisema maandalizi ya mashindano hayo, yanaendelea vizuri na katika kuhakikisha wanafanikisha mashindano hayo wameunda kamati tatu ziatakazokuwa na jukumu la kuyaiwezesha michuano hiyo.

Alizitaja kamati hizo kuwa ni Kamati ya Mipango, Kamati ya Fedha na Kamati ya Mapokezi ambazo zinaundwa na wajumbe kutoka BFT na wengine kutoka klabu zitakazoshiriki.

No comments:

Post a Comment