Na Elizabeth Mayemba
KOCHA Mkuu wa Simba, Mzambia Patrick Phiri ameanza kutafuta mikanda (DVD) ya fainali ya michuano Klabu Bingwa ya Dunia kati ya TP Mazembe na
Inter Milan, ili aweze kuitumia katika maandalizi ya timu yake.
Simba inatarajia kucheza mchezo wa mzunguko wa pili wa Klabu Bingwa Afrika, dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Machi 18 na 20 mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana Meneja wa Simba Innocent Njovu, alisema kocha huyo kuna mkanda ambao anatarajia kuupa hivi karibuni kwa ajili ya kuutumia wakati timu yake ikijiandaa kupambana na TP Mazembe.
"Kocha kasema kuna mkanda ambao anatarajia kuupata muda wowote kuanzia sasa, sijui ni mkanda gani lakini alisema akiupata wa fainali ya Klabu Bingwa Dunia kati ya TP Mazemba na Inter Millan, utamsaidia sana," alisema Njovu.
Alisema kocha anataka kuhakikisha anaandika historia kwa kuifunga timu hiyo na ndiyo maana, amekuwa akihangaika kupata mkanda wake ili kusoma mbinu za wapinzani wao.
Njovu alisema timu yao imeanza kufanya mazoezi ya ufukweni jana asuhuhi na leo wataanza kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu ya Bara dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Jumapili.
Alisema maandalizi ya mchezo huo yanakwenda vizuri na makosa yaliyojitokeza katika mechi iliyopita, kocha atayafanyia kazi ili waibuke na pointi tatu.
No comments:
Post a Comment