Na David John
SERIKALI ya Marekani kupitia Shirika lake la Misaada (USAID) kwa kushirikiana na shirika lisilokuwa la kiserikali nchini Engender Health kupitia mradi wa
Champion wamezindua programu mpya kwa wanandoa kujenga tabia ya kupima UKIMWI na kupanga uzazi ili kujenga familia iliyo bora.
Akizungumza Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa programu hiyo jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Bi. Blandina Nyoni alisema kuwa virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi ni moja ya matatizo makubwa kwa Tanzania na hii inatokana na kutokuwa na tabia ya kupima mara kwa mara na wanandoa kutokuwa na uaminifu katika mahusiano yao ndani ya nyumba.
"Kupitia Valentine Day (Siku ya wapendanao) nawaasa Watanzania hasa wanandoa kukaa pamoja kupanga malengo yao na kuwa waaminifu katika ndoa na kujenga tabia ya kupima mara kwa mara na kushirikishana katika maamuzi mbalimbali ndani ya nyumba," alisema.
Pia alisema katika utafiti uliofanywa kuhusiana na Ukimwi pamoja na malaria mwaka 2007 na 2008 ilionyesha asilimia 6.6 kwa wanawake walio katika ndoa wameathiriwa na tatizo wakati kwa wanaume ni asilimia 4.6.
Mwakilishi kutoka Marekani, Bi. Jens Schules alisema nchi yake kwa kutambua jitihada za serikali ya Tanzania wanaunga mkono na kusaidia katika kupambana na Ukimwi pamoja na malaria kupitia mradi wa Champion, na kuwataka Watanzania kutumia siku ya wapendanao kukaa pamoja kupanga mambo mbalimbali ya kimaendeleo ikiwa pamoja na uzazi ili kujenga familia iliyo bora.
No comments:
Post a Comment