Na Omari Moyo, Arusha
MADIWANI 12 wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kusikiliza kilio chao kikubwa cha uhaba wa ardhi kwa ajili ya
kilimo, ufugaji na makazi katika kwenye wilaya hiyo.
Mgogoro huo wa uhaba wa ardhi kwenye wilaya hiyo umesababisha mapigano ya mara kwa mara kwenye eneo hilo kati ya wafugaji na wakulima wakigombea ardhi ama ya kilimo au kwa ajili ya mifugo na kusababisha vifo na vilema vya maisha.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Ngorongoro, Bw. Elias Ngorisa alisema kuwa wameamua kumuomba rais kulishughulikia suala hilo kwa kuwa yeye pekee ndiyo mwenye mamlaka ya mwisho kwenye matumizi ya ardhi.
“Rais ndiyo ataamua kutupa eneo lolote ndani ya wilaya yetu kwa ajili ya kilimo, ufugaji ama makazi, kwani eneo letu limezunguikwa na maeneo mengi ya watu waliojimilikisha wakiwa hawayatumii kama kanuni za ardhi zinavyoelekeza,†alisema Ngorisa.
"Lengo la kwenda kwa Rais Kikwete ni kwenda kumweleza tatizo la ardhi ambalo wakati wa kampeni aliahidi kulitafutia ufumbuzi, sasa baada ya mapigano yanayoendelea tumeona ni wakati mwafaka wa kumkumbusha na kuiomba serikali kuacha kutupuuza," alisema.
Migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo inatokana na sehemu kubwa kuwa hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro na sehemu iliyobaki kuwa pori tengefu la Loliondo.
Wiki moja iliyopita kulizuka mapigano ya kugombea ardhi kati ya wakulima na wafugaji na mtu mmoja alifariki na wengine kadhaa kujeruhiwa.
No comments:
Post a Comment