15 February 2011

'Utawala bora kwa klabu ni donda ndugu'

Na Zahoro Mlanzi, Aliyekuwa Bagamoyo

SERIKALI imesema utawala bora kwa klabu za Ligi Kuu ni sawa na donda ndugu kwani kila kukicha huandamwa na migogoro kuliko kupanga
mikakati ya kuendeleza soka nchini.

Kauli hiyo ilitolewa mjini Bagamoyo jana na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Iddi Kipingu, kabla ya kufungua semina iliyoandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kwa viongozi wa juu wa klabu za Ligi Kuu.

Kipingu alisema klabu za Tanzania zinatumia muda mwingi katika migogoro kuliko maendeleo ya timu na ndilo jambo linalosababisha klabu nyingi kushindwa kufanya vizuri katika michezo ya kimataifa.

"Naomba viongozi mliopo hapa, muichukulie hii semina kwa umakini sana, kwani elimu ya utawala bora mtakayoipata hapa mkiitumia vizuri hakuna ubishi, tutayaona matunda yake," alisema Kipingu.

Alisema ukiwa na uwezo wa kiutawala hata fedha ukipewa na mdhamini, utajua jinsi ya kuzitumia, lakini kinachofanyika sasa, klabu zinadhaminiwa kwa mabilioni ya fedha, kinachofanyika hakuna.

Alisema fedha za mdhamini zitaonekana zina faida endapo zitatumika vizuri na sio zilete mgogoro ndani ya klabu.

Naye, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, alisema maadhimio yaliyofikiwa miaka mitatu iliyopita, yasipofikiwa huenda timu za hapa nchini hazitashiriki katika michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Elimu na Ofisa Maendeleo ya Ufundi kutoka FIFA, Jaques Male, aliipongeza timu ya Simba kwa kufuzu hatua ya pili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Alisema ni nafasi nzuri kwa Simba sasa, kucheza na TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuonesha uwezo wao na kuipa pole Yanga na kuitaka iongeze bidii katika michuano ya kimataifa.

Simba itakutana na TP Mazembe katika hatua ya pili baada ya kuichapa Elan de Mitsoudje ya Comoro mabao 4-2, Yanga wao ilitolewa na Dedebit ya Ethiopia kwa mabao 6-4.

No comments:

Post a Comment