21 February 2011

Tushirikiane kuhubiri amani-Dkt. Bilal

Na Mwandishi Maalumu

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal ametoa wito kwa Watanzania kushirikiana kuhubiri amani
ili kuhakikisha kuwa haitoweki nchini.

Dkt. Bilal alitoa wito huo jana wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Istiqaama nchini katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

"Kwa hiyo, kila mmoja wetu katika jamii hana budi kuhakikisha kwamba amani katika nchi yetu haitoweki. Wito wangu kwenu nyote ni kwamba tusaidiane ili kuhubiri amani. Tuilinde nchi yetu," alisema.

Makamu wa Rais aliwaeleza waumini waliohudhuria maadhimisho hayo kuwa kwa wale wasiojua raha ya amani wanapaswa kuangalia shida za watu wanaoishi katika nchi zisizo na amani.

"Tukitaka kujua raha ya amani tuangalie shida ya nchi ambazo hazina amani. Watu wanateseka na hakuna hatua zozote za maendeleo zinazofikiwa, aliongeza.

Dkt Bilal aliipoongeza Taasisi ya Istiqaama nchini kwa kuwa na mipango mizuri ambayo imelenga kuboresha hali ya maisha ya Watanzania, ikiwamo ujenzi wa hospitali ya kisasa, shule, maktaba kubwa na ya kisasa pamoja na vituo vya kuelelea watoto.

Jambo hili litasaidia sana serikali kufikisha huduma zake kwa jamii, kwani hili si jukumu la serikali pekee yake bali ni kila mwenye uwezo.Juhudi hizi za Jumuiya ya Istiqaama bila shaka zitasaidia jamii kuondokana na umasikini na kupata maendeleo
endelevu.

Wakati huo huo Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Shekhe Mussa Soraga amewataka wananchi wa Tanzania bara wasikatishwe tamaa na baadhi ya watu wanaoweza kubeza jitihada za madhehebu ya dini mbali mbali ya kukaa pamoja kushirikiana katika kulinda na kuendeleza amani nchini.

Wapo wanaoweza kuzibeza juhudi zenu hasa miongoni mwetu waislamu kwa kuwalaumu kwa nini mnashirikiana na watu wa dini nyingine, lakini hilo liwavunje moyo kwani ni sisi viongozi wa dini tunaoweza kudhibiti nyoyo za waumini wetu na tukifanikiwa
kufanya hivyo amani yetu itadumu, alisema Shekhe Soraga.

Waumini waliohudhuria maadhimisho hayo walichangia jumla ya sh. 11,687,000.00 kwa ajili ya kuwasaidia wananchi walioathirika na milipuko ya Gongolamboto.

1 comment:

  1. Kwa heshima na taadhima napenda kumpongeza Makamu wa Rais Dk. Bilal pamoja na viongozi wa Dini ya Kiislamu. Japo mimi si mwislamu lakini kuna ndugu zangu wengi wa kuzaliwa ni Waislamu na kwa ajili hii mimi nimekulia ndani ya jamii yenye mchanganyiko wa imani. Wakati wa Ramadhani nifikapo kwa ndugu zangu basi kwa kuwa huwa wamefunga siwalazimishi kunisongea ugali, ila shemeji hunisongea pembeni mchana akijua ya kwamba nina njaa kitu ambacho kwake si kikwazo. Na jioni kwenye kufturu hukaribishwa. Kama Mheshimiwa Makamu wetu wa Rais alivyotuomba Watanzania kuhubiri AMANI nasema Mwenyezi Mungu na awajalie viongozi wetu wa Serikali, Mashirika, Madhehebu kuziondoa tofauti zao. Na amani ya kweli huanzia ndani ya familia, na jamii. Niseme kwa moyo wa heshima kuwashukuru waumini waliohudhuria maadhimsho hayo na kukumbuka kutoa swadaka(mimi naiita swadaka)na wala si mchango tu kwa ajili ya walioathirika na milipuko Gongo la Mboto. Mwenyezi Mungu Maulana awajalie na awazidishie,

    ReplyDelete