Mwandishi Wetu
SUALA la serikali kukatisha mkataba kati yake na Kampuni ya A to Z Textile Mills wa kupunguza matawi ya miti kwenye msitu wa Meru/Usa limeingia katika
sura mpya baada ya kuonekana dalili za kuupitia upya ili kuweka mazingira ya usawa kimaslahi kwa pande zote mbili
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Ladislaus Komba alisema hayo jana kwa njia ya simu kutoka Dar es Salaam huku akikanusha taarifa zilizotolewa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kwamba kampuni hiyo ilikuwa inakata magogo badala ya kukata matawi.
Mkataba ulisitishwa kwa muda ili kuwezesha serikali na kampuni hiyo kuupitia ili kuwezesha pande zote mbili kufaidika. Ila taarifa kwamba kampuni ilikuwa inafanya kazi isivyo halali ni uwongo, alisema.
Pia alikanusha taarifa kwenye vyombo vya habari kwamba Waziri Ezekiel Maige alisema kwamba kampuni hiyo ilikuwa inatumia mkataba feki katika kupunguza matawi ya miti.
Alichosema waziri ni kusitishwa kwa muda kwa mkataba ambao ni halali ili kuweza kuupitia tena, alisema.
Dkt. Komba aliitaka kampuni hii kupeleka malalamiko yao serikalini endapo kusitishwa kwa mkataba huo kutasababisha hasara kwa kampuni.
Kwa upende wake, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya A to Z Textile Mills, Bw. Anuj Shah alisema shutuma zilizotolewa dhidi ya kampuni yake kwamba inafanya kazi chini ya mkataba tata hazina msingi na ni uongo kutokana na jinsi kampuni inavyothamini na inavyochukulia kwa umakini suala la utunzaji wa mazingira na ndio maana waliamua kupunguza matawi badala ya kununua magogo.
Narudia tena kwamba ni uongo mtupu kwamba malori ya kampuni yetu yalikutwa na waziri yakiwa yamesheheni magogo wakati alipofanya ziara fupi, alisema.
Kampuni yetu inasikitishwa sana na shutuma hizi za uongo ambazo zimeharibu sifa nzuri ya kampuni, ukizingatia kwamba walioandika hawakuwasiliana na sisi ili kupata maelezo ya kampuni kuhusu suala hili,†alisema.
Bw. Shah alimwomba waziri aondoe pingamizi la kusitishwa kwa mkataba huo wakati wakati ukiwa unapitiwa ili kufanya kampuni iweze kuendelea na uzalishaji.
Tumeajiri watu zaidi ya 8,000 hivyo usitishwaji wa ghafla wa mkataba huo utasababisha kufungwa kwa kiwanda na kuleta madhara makubwa sio tu kwa waajiriwa bali hata wale wanaowategemea,†alisema.
Alitetea uamuzi wa kampuni kulipa sh. 1,000 kwa tani moja ya kuni kutokana na matawi ya miti kwamba gharama nyingine zinazoendana na zoezi hilo ni lazima zijumuishwe pamoja.
Tani moja ya kuni kutoka kwenye matawi yaliyopunguzwa kwenye miti ni zaidi ya sh. 45,000, kumbe sio sahihi kung'ang'ania kwamba kiasi cha sh. 1,000 ni kidogo bila kuangalia gharama nyingine. Pia barabara za kuelekea kwenye misitu zimeboreshwa sana na pia zaidi ya vijana 250 wamepata ajira kwenye kazi ya kupunguza matawi, alisema.
Alisema kampuni ingeweza kutumia 40,000/- kununua tani moja ya magogo kwa ajili ya kuni ambazo huuzwa na watu binafsi, lakini kutokana na dhamira chanya ya kampuni ya kutaka kutunza mazingira ndio sababu iliyopelekea uamuzi wa kujiingiza kwenye upunguzaji wa matawi.
Alisema kampuni yake iliombwa ipunguze matawi ya miti baada ya serikali kushindwa kufanya shughuli hiyo kwenye miaka ya 1990 kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha.
Watanzania tumelaaniwa au ni vipi jamani?
ReplyDeleteKarne hii tunaruhusu viwanda vinavyotumia nishati ya kuni?
Hii haifai kabisa wenye hicho kiwanda watumie nishati mbadala.
Hizo ajira tunazofikiri zinatusaidia huenda sio kweli kama hatutaachana na matumizi ya kuni kwenye kiwanda kikubwa kama hiki.
Kama kiwanda kinaruhusiwa kutumia kuni ina maana hata kuchoma mkaa ni ruksa au?
Wataalamu wa mazingira mko wapi?
Sisi tuko karibu na hiki kiwanda tunaona mizigo mingi mno ya kuni ikiigizwa kiwandani kila siku.
Mimi ninashauri wafute kabisa huo utaratibu wa kutumia kuni.