15 February 2011

Tamim arejea kumkabili Ashraf

Na Victor Mkumbo

BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Awadh Tamim, ametamba kumchapa Ashraf Suleiman wa Zanzibar, katika pambano la uzito wa juu
litakalofanyika kwenye ukumbi Diamond Jubilee, Machi 5, mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam jana, akitoke nchini Sweden, Tamim alisema kuwa, anatarajia kumpiga mpinzani wake katika raundi za mwanzo ili aweze kuendeleza rekodi yake ya ushindi.

Alisema pambano hilo linatarajiwa kuwa na upinzani mkali, lakini kutokana na maandalizi aliyofanya, anatarajia kushinda kwa KO.

Alisema pambano hilo litakuwa la ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati la uzito wa juu, la raundi 10.

Alisema akiwa bingwa wa mkanda huo Afrika Mashariki na Kati, aliutwaa baada ya kumchapa mpinzani wake Thomas Ukusi wa Kenya.

"Nimerejea nchini kwa ajili ya pambano langu na Ashraf, mara ya kwanza tulipigana na pambano lilivunjika, hivyo ninatarajia kufanya kweli kwa kumchapa kwa KO," alisema.

Alisema katika kipindi alichokaa Sweden, alifanikiwa kucheza mapambano matatu na kushinda mawili, ambapo moja alichapwa.

Naye, Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya AURORA, Shomary Kimbau, alisema maandalizi ya pambano hilo yamekamilika.

Alisema wanampongeza Tamim kwa kurejea tena nchini kwa ajili ya pambano hilo, ambalo la kutetea ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati.

No comments:

Post a Comment