14 February 2011

Simba yametimia

*Sasa kukutana na TP Mazembe

Na Zahoro Mlanzi

HATIMAYE sasa yametimia, unaweza kusema hivyo, baada ya mabingwa wa soka Tanzania Bara, timu ya
Simba, kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Elan de Mitsoudje ya Comoro,  katika mchezo wa Klabu Bingwa Afrika uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, jana.

Kwa ushindi huo, Simba sasa itaumana na mabingwa watetezi wa michuano hiyo, TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), katika hatua inayofuata.

Tangu ratiba ya michuano hiyo ilivyotolewa kwa mara ya kwanza na kuonesha Simba ikivuka hatua ya awali itaumana na Mazembe, mashabiki na wanachama wa timu hiyo, walikuwa wakiomba kwa udi na uvumba wakutane nayo, na jambo hilo limetimia.

Katika mchezo huo wa jana ambao ulihudhuriwa na mashabiki wengi, huku wengine kubaki nje ya uwanja kutokana na uwanja huo kujaa, ulianza kwa kasi huku kila timu ikicheza kwa tahadhari zaidi.

Ilikuwa ni Simba iliyokuwa ya kwanza kubisha hodi langoni mwa Mitsoudje, baada ya Ali Ahmed 'Shiboli' kumzidi ujanja Othouman Ibrahim na kupiga krosi iliyokosa mmaliziaji na mpira kutoka nje.

Simba iliendeleza mashabulizi langoni mwa Mitsoudje na dakika ya 12, Shiboli nusura aifungie Simba bao la kwanza, baada ya kuunganisha vibaya krosi iliyopigwa na Rashid Gumbo na mpira kutoka pembeni ya goli.

Mitsoudje ilitulia na kupanga mashambulizi, ambapo dakika ya 30, Madaha Mohamed alitoa pasi fyongo kwa Mousteckima Mohamed, baada ya kubaki na beki Kelvin Yondani, lakini kipa Juma Kaseja aliuwahi na kuudaka.

Mitsoudje iliongeza mashambulizi kwa Simba na dakika ya 43, Madaha aliifungia timu yake bao la kwanza kwa shuti lililotinga moja kwa moja wavuni, baada ya mabeki wa Simba kudhani ameotea.

Mbwana Samatta wa Simba aliisawazishia timu yake, ikiwa imebaki dakika moja kabla ya kipyenga cha mapumziko kupulizwa, kwa shuti lililombabatiza Youssouf Mohamed na kutinga wavuni.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, dakika ya pili tangu kipindi hicho kianze, Patrick Ochan, aliifungia Simba bao la pili, baada ya kuugonga mpira uliopigwa na Samatta na kutinga wavuni.

Baada ya kufunga bao hilo, Simba iliongeza lingine dakika ya 56, lililofungwa na Samatta, baada ya kuanziwa mpira wa adhabu na Juma Jabu, na kupiga shuti nje ya eneo la hatari lililoshindwa kudakwa na kipa Youssouf Ahamada.

Mitsoudje ambayo inacheza soka la chini chini na kupiga pasi nyingi, dakika ya 63, ilifunga bao la pili kupitia kwa Abdulhouda Abdoleafor kwa shuti, baada ya wachezaji wenzake kuonana vizuri na kumpasia mfungaji.

Timu hizo ziliendelea kuonesha kandanda safi kwa kushambuliana kwa zamu, dakika ya 72, Amri Kiemba wa Simba aliyeingia badala ya Shiboli, aliifungia timu yake bao la mwisho akimalizia krosi iliyopigwa na Haruna Shamte kutokana na mabeki kudhani ameotea.

Simba: Juma Kaseja, Haruna Shamte, Juma Jabu, Juma Nyosso, Kelvin Yondani, Mohamed Banka/Jerry Santo, Rashidy Gumbo/Shija Mkina, Patrick Ochan, Mbwana Samatta, Ali Ahmed/Kiemba, Mussa Hassan 'Mgosi'.

1 comment:

  1. TP Mazembe ni mabingwa watetezi wa vilabu Barani Afrika na makamu bingwa wa Dunia ngazi ya vilabu,Simba wanapaswa kuanza maandalizi ya uhakika kiufundi,kisaikolojia na kiuongozi.

    ReplyDelete