14 February 2011

Phiri aivutia pumzi TP Mazembe

Na Zahoro Mlanzi

BAADA ya kuifunga Elan de Mitsoudje kutoka Comoro katika mchezo wa Klabu Bingwa Afrika, Kocha Mkuu wa wabingwa wa
soka Tanzania Bara, Simba, Patrick Phiri, ametamba kuwafunga mabingwa watetezi wa michuano hiyo, TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), nyumbani.

Kauli hiyo ya Phiri aliizungumza muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliopigwa jana, Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 4-2.

Phiri alisema michuano hiyo ndio kwanza inaingia katika hatua ya pili, hivyo ni mapema kuanza kuzungumzia hali ya baadaye, kwani kila timu ina nafasi ya kutwaa ubingwa.

"Naiheshimu TP Mazembe, ni timu bora Afrika na si Afrika hata kwa Dunia kwani ilifika fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia, licha ya kuwa na ubora huo, nina imani hapa nyumbani tutaibuka na ushindi," alisema Phiri.

Alisema kikubwa kinachotakiwa ni kufanya maandalizi ya kutosha kwani mchezo huo dhidi ya Mazembe ni mchezo mgumu kwao.

Akizungumzia mchezo huo wa jana, Phiri alisema anawashukuru wadau, wanachama na wapenzi wa soka nchini kwa kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu yao.

Alisema soka la Comoro limepiga hatua kubwa, licha ya kuibuka na ushindi huo, mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa kiasi kilichompa wakati mgumu kocha huyo.

Alisema kama si juhudi za wachezaji wake katika kuhakikisha wanawatuliza Wacomoro hao, ingekuwa ngumu kuvuka hatua hiyo.

No comments:

Post a Comment