Na Zahoro Mlanzi
ZIKIWA zimebaki siku 26 kabla ya mabingwa wa soka Tanzania bara, Simba kuumana na TP Mazembe, uongozi wa timu hiyo umesema benchi la
ufundi ndilo litakaloamua kama wacheze michezo ya kirafiki ya kimataifa au vinginevyo kabla ya kuumana na timu hiyo.
Benchi hilo linaongozwa na Kocha Mkuu, Patrick Phiri akisaidiana na Amri Said watakuwa na kazi ya ziada kuhakikisha wanaiandaa vizuri timu hiyo ili iiondoshe Mazembe katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Wakati Phiri akitafakari hilo, tayari vyombo vya habari vimeripoti kwamba huenda timu hiyo ikapiga kambi nchini Zambia kabla ya kwenda Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kucheza na Mazembe.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Cliffold Ndimbo alisema maandalizi kwa ajili ya klabu bingwa yanaendelea na kwamba uongozi unasubili mapendekezo kutoka kwa benchi la ufundi.
"Maandalizi yanaendelea ila kwa sasa tunachosubili ni taarifa kutoka benchi la ufundi kama litahitaji mechi za kirafiki za kimataifa au la na baada ya kupokea ndipo sasa tutakaa na kujadili," alisema Ndimbo.
Alisema pamoja na kusubili taarifa hizo, michezo ya Ligi Kuu bara nayo itakuwa ni sehemu ya maandalizi yao katika kuhakikisha wanaing'oa timu hiyo na kuweka historia mpya.
Ndimbo alisema leo wataendelea na mazoezi kama kawaida kwani wanajiwinda na mchezo mgumu dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa Jumapili ijayo.
Akizungumzia hali za wachezaji wao, alisema wachezaji wote wapo katika hali nzuri ila Uhuru Seleman na Hilary Echessa bado hali zao hazijatengemaa.
No comments:
Post a Comment