*Yazishusha Yanga, Simba kileleni
Na Zahoro Mlanzi
TIMU ya Azam FC, imekwea mpaka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara baada ya kuifunga
JKT Ruvy ya Pwani mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Azam sasa imefikisha pointi 35 sawa na waliokuwa vinara wa ligi hiyo, Yanga ila inaongoza kwakuwa na uwiano mzuri wa mabao ukilinganisha na Yanga.
Kabla ya mchezo wa leo, Azam ilikuwa ikiongoza kwa tofauti ya mabao 19 na sasa itakuwa na mabao 21, Yanga ina mabao 18 na Simba ambayo ipo katika nafasi ya tatu kwa pointi 34 ina mabao 14.
Katika mchezo huo wa jana, timu zote zilianza mchezo kwa kukamiana kwa kuchezeana faulo na kutumia nguvu nyingi lakini Azam ilikuwa ya kwanza kubisha hodi langoni mwa JKT dakika ya 15 baada ya John Bocco na Mrisho Ngassa kuonana vyema lakini shuti la Bocco lilitoka nje.
JKT iliyoonekana kutawala mchezo huo kwa kupiga pasi nyingi, dakika ya 30, Bakari Kondo alishindwa kuifungia timu yake bao baada ya kubaki na Luckson Kakolaki ambapo alipiga shuti dhaifu na kutua mikononi mwa kipa Jackson Chove.
Ikiwa zimebaki dakika tatu kabla ya mchezo kuwa mapumziko, Ibrahim Mwaipopo aliifungia Azam bao la kwanza kwa shuti nje ya eneo la hatari baada ya kupokea pasi iliyotolewa kwa kifua na Bocco na kutumbukiza mpira wavuni.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo dakika ya 59, Azam ilipata pigo baada ya Mwaipopo kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kumchezea vibaya Kondo.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana huku JKT ikitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini washambuliaji wake walishikwa ma kigugumizi cha miguu kila walipolikaribia lango la Azam.
Dakika ya 73, Shaibu Nayopa wa JKT katika harakati za kuokoa hatari golini kwake alijikuta akitumbukiza mpira wavuni kutokana na kona iliyopigwa na Ibrahim Shikanda na kufanya dakika 90 zikimalizika Azam kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Katika michezo mingine ya ligi hiyo, jijini Mwanza, Mwandishi Wetu, Daud Magessa anaripoti kwamba wenyeji Toto African imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Arusha FC.Mabao ya Toto yalifungwa na Hussein Swedi na Semmy Kessy na la AFC lilifungwa na Abdallah Juma.
Katika mchezo mwingine uliopigwa Kagera, Mwandishi Wetu, Theonista Juma anaripoti kwamba wenyeji Kagera Sugar ilitoka suluhu na African Lyon katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Kaitaba mkoani humo.
No comments:
Post a Comment