28 February 2011

Shivji alipu ufisadi kwenye majengo

Na Gladness Mboma

BAADHI ya majengo makubwa nchini yamedaiwa kujengwa kwa kutumia fedha za walanguzi na mafisadi na fedha zinazopatikana kutokana na pango
zinahamishiwa nchi za nje kwa kigezo cha uwekezaji.

Profesa Issa Shivji wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akitoa mada iliyokuwa inahusu ardhi na ulinzi wa rasilimali katika katiba kwenye kongamano liloandaliwa na Asasi ya HakiArdhi.

Prof. Shivji alisisitiza kwamba magorofa makubwa yanayojengwa Tanzania yanajengwa na fedha za walanguzi, wanaiba fedha kutoka Tanzania wanapeleka Dubai na kisha wanarudisha fedha kiduchu na kazi kubwa ya viongozi nchini ni kuyazindua.

Alisema kuwa utakuta matajiri wanatoka Dubai wanakuja kupora ardhi na kuhamishia utajiri wote kwao na kuwa, kilichobaki sasa ni kuanza kupora mito na milima.

"Kumekuwa na uporaji wa ardhi ya kijiji na wawekezaji mafisadi wa ndani na nje kwa visingizio mbalimbali kama kilicho kwa ajili ya kuzalisha nishati, na uzalisha wa mazao ya chakula kwa ajili ya masoko ya kimataifa," alisema.

Alisema kwa miaka 50 baada ya uhuru wananchi wengi hawana haki ya kupata ardhi badala yake wawekezaji ndiyo wameipata na wamekuwa wakitumia kupora utajiri wa nchi.

Prof. Shivji alisema kuwa uporaji huo wa ardhi umesababisha maisha kuwa magumu, bei za vyakula zimepanda kwa sababu ya wananchi kukosa nafasi ya kuzalisha tena.

"Ninashauri wananchi washirikishwe katika kujadili mfumo mpya wa katiba utakaotoa fursa kwa wananchi ili wawe na nguvu ya kumiliki ardhi na rasilimali zao," alisema.

Alisema kwamba katiba ya sasa haisemi lolote kuhusu ardhi badala yake imegusia haki ya wananchi kumiliki ardhi na kusababisha utata kuhusu umilikishaji wa ardhi.

Prof. Shivji alisema madai na matakwa ya wanakijiji na wananchi waliowengi kuhusu ardhi na rasilimali zao yawe mstari wa mbele katika mjadala wa kitaifa kuhusu katiba mpya.

Naye Bw. Odenda Lumumba kutoka Chama cha Watetezi wa Ardhi Kenya alitoa uzoefu wa masuala ya ardhi na jinsi ilivyoingizwa kwenye mabadiliko ya katiba mpya ya nchi yao, alisema kuwa walianza mjadala wa muda mrefu na baadaye walifanikiwa.

Alisema kuwa wao waliandaa mapendekezo yao na kuyapeleka kwenye mchakato wa katiba na asilimia 90 ya mapendekezo yao yamepitishwa na kuwataka Watanzania kutolala usingizi katika hilo.

Bw. Bashiru Ally, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliwataka Watanzania wasisubiri kengele ya mwezi wa nne wakati muswada wa mijadala kuhusu katiba utakapopelekwa bungeni, bali waanze kuijadili sasa.

"Kuna wasiwasi wa wananchi kutoshirikishwa katika mjadala wa katiba na badala yake unaweza ukatekwa nyara," alisema.

2 comments:

  1. Profesa
    Nakushukuru kwa mada yako. hiyo haipingwi ila niwakati chini ya ushauri wako utueleze tufanye nini ili kunusuru nchi. Pia waeleze viongozi walioko madarakani kwamba itakuwa aibu kwao pale wananchi watakapoamua kudai hai yao ya ardhi kwa nguvu walizo nazo, kwani itakuwa na madhara makubwa kwao na wagani jambo ambalo litakuwa ni aibu kubwa. najaribu kuangaliya yanayofanyika kwenye nchi za kiarabu na kujiuliza endapo wenye maisha bora zaidi yetu wamechoka na mambo wanayofanyiwa, itakuwaje maskini hohehahe wakiamua????????? oh. hatari iko mbele na tutashindwa kujitetea. labda uwashauri wageni waanze kuondoka kungali mapema na waiogope ardhi yetu.

    ReplyDelete
  2. Watanzania wameshaporwa sana na wataporwa sana. Tuliamua kumpa kichaa rungu, nasi akifanya makeke yake tunafurahia, tunasema atapona tu! Haponi. Mungu wangu angalia majengo yote ya kihistoria hasa Dar es salaam, yanavunjwa kwa kisingizio kuboresha mji. Kumbe kuua ajira, kupaunguza watalii na fedha za kigeni, kuwapata maeneo muhimu wageni. Angalia inakuwaje mahakama ya rufaa inampa mtu jengo la kihistoria eti lijengewe jengo jipya. Upumbavu mtupu

    ReplyDelete