28 February 2011

Shein: Tumeshaanza kupambana na umasikini

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein amesema Serikali ya aawamu ya Saba tayari imeanza kupambana na tatizo la umasikini na ukosefu wa
ajira kwa kushirikiana na nchi wahisani.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kibandamaiti juzi, Dkt. Shein aliwaeleza wanachama wa CCM wa mikoa mitatu kuwa tayari mfuko wa kupambana na umasikini na kuwajengea uwezo vijana umezinduliwa na wizara maalumu iliyoanzishwa ya kuwawezesha wananchi wake.

Alisema tayari Serikali ya Norway imejitokeza kuchangia mfuko huo kwa kutoa sh. milioni 140 fedha ambazo zitawasaidia wajasiriamali na vijana katika kuondokana na tatizo la ajira na kuwataka vijana kutumia fursa hiyo iliyoanzishwa na serikali.

"Serikali yenu imeshanza kutekeleza badhi ya ahadi zake na hivi karibuni kumezinduliwa mfuko wa vijana, ambapo vijana hao wataweza kuongwezewa nyenzo za kuwawezesha kujiajiri wenyewe na kuendeleza mitaji yao," alisema Dkt. Shein.

Kuhusu utawala bora alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa itatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia utawala wa sheria na kutoa onyo kuwa hatowavumilia watu wababe wasiozingatia sheria katika utawala wake.

Alisema lengo la kuanzisha Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala bora ni kuongeza uwajibikaji na kuona watu wote wanakuwa sawa mbele ya sheria na kuwataka wananchi waondoe hofu
kuhusu serikali yake hasa katika kufikia malengo ya utekelezaji ya ilani ya uchaguzi na kujenga umoja wa kitaifa.

Alisema kuwa Zanzibar imepata sifa kubwa baada ya kufikia maelewano
yaliyoleta Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kumpongeza rais Mstaafu, Amani Abeid Karume kwa hatua mbali mbali alizozichukua za kujenga misingi ya kisiasa na kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar.

Hata hivyo alisema wanachama wa CCM wanapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuangalia kasoro zilizosababisha kupoteza viti vitatu likiwemo jimbo la Nungwi, jambo ambalo alisema lisingetokea kama wana CCM wangalikuwa na msimamo mmoja katika kuchagua wagombea wakati wa kura za maoni.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, Mke wa Rais Mama Mwema Shein, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Bw. Saleh Ramadhan Ferouzi na viongozi wengine wa nchi.

No comments:

Post a Comment