28 February 2011

Simba yainyoosha Mtibwa

*Yakalia tena usukani wa ligi

Na Zahoro Mlanzi

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba jana ilikalia tena usukani wa ligi hiyo baada ya kuinyuka Mtibwa Sugar mabao 4-1, katika
mechi iliyopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Usukani wa ligi hiyo, sasa umekuwa kama mbio za kupokezana vijiti kwa timu za Simba, Yanga na Azam FC ambazo zimekuwa zikipokezana kila mara.

Kwa matokeo hayo, Simba sasa inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 37, ikifuatiwa na Azam FC ambayo ina pointi 35 sawa na Yanga yenye pointi kama hizo, lakini ikizidiwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Simba ilipata bao la kwanza dakika ya 13 kupitia Mbwana Samatta, ambaye alipiga shuti lililogonga mwamba na kutinga wavuni baada ya kupokea pasi ya Amri Kiemba.

Kabla ya kuingia kwa bao hilo, Simba ilitikisa nyavu dakika ya tatu kupitia kwa Kiemba, ambalo hata hivyo mwamuzi alilikataa kwa madai kuwa Shija Mkina wa Simba, alimfanyia madhambi kipa Omary Ally kabla ya mpira kujaa wavuni.

Mchezo ulilazimika kusimama kwa dakika tano kutokana na kipa huyo kufanyiwa matibabu, lakini hata hivyo alishindwa kuendelea na mchezo na kutolewa nje kwa machela huku nafasi yake ikichukuliwa na Soud Slim.

Baada ya kushambuliwa mfululizo, Mtibwa Sugar ilizunduka na kuanza kuliandama lango la Simba, ambapo Salum Machaku nusura aifungie timu yake bao kutokana na shuti lake kugonga mwamba wa juu na kudunda ndani lakini hata hivyo, mlinzi Juma Jabu aliondosha hatari hiyo.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuingia na uchu wa kufunga mabao na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 46, lililofungwa na Kiemba akiunganisha krosi ya Rashid Gumbo, aliyeingia badala ya Hilary Echesa.

Mtibwa ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 55, kupitia kwa Hussein Java, baada ya kuunganisha krosi ya Machaku ambaye alimpiga chenga beki Juma Nyoso.

Dakika ya 66 Samatta, aliipatia Simba bao la tatu baada ya kuruka mbizi na kuupiga mpira kichwa akiunganisha krosi, iliyochongwa na Mkina.

Samatta aliiandika Simba bao la nne na la tatu kwake katika mechi hiyo kwa mkwaju wa penalti, baada ya kipa wa Mtibwa, Slim kumkwatua Mussa Hassan 'Mgosi', aliyeingia kuchukua nafasi ya Nico Nyagawa.

Ligi hiyo itaendelea tena leo katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kati ya Yanga na Ruvu Shooting na endapo Yanga itashinda itakuwa inaongoza.

No comments:

Post a Comment